Dar es Salaam. Serikali imeieleza Mahakama kuwa, bado inaendelea na uchunguzi katika kesi ya kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine na methamphetamine zenye uzito wa kilo 447.3 inayowakabili raia wanane wa Pakistani.
Kwa pamoja, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka mawili ya kusafirisha dawa hizo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa hao ni Mohamed Hanif (50), Mashaal Yusuph (46), Imtiaz Ahmed (45), Tayab Pehilwam (50) maarufu kama Tayeb na Immambakshi Kudhabakishi(55).
Wengine ni Chandi Mashaal (29), Akram Hassan (39) na Shehzad Hussein (45).
Wakili wa Serikali, Erick Kamala ameieleza Mahakama hiyo leo Jumatano Januari 22, 2025 wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Wakili Kamala amedai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea.
“Kutokana na upelelezi wa kesi hii kutokamilika, tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” aliomba wakili Kamala.
Hakimu Nyaki alikubaliana na upande mashtaka na kuahirisha kesi hiyo hadi Februari 4, 2025 kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili, hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.
Hata hivyo, kutokana na washtakiwa hao kutokujua Kiswahili wala Kingereza, Mahakama imelazimika kutafuta mkalimani wa kutafsiri kila kinachoelezwa kwa Urdu, lugha inayotumika nchini Pakistani.
Mkalimani huyo, Salma Mohamed, raia wa Pakistani, alifanya tafsiri kutoka Kiingereza kwenda lugha ya Urdu.
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo, Januari 9, 2025 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi namba 395 ya mwaka 2025.
Katika shtaka la kwanza, washtakiwa wanadaiwa kusafirisha kemikali ya kutengenezea dawa.
Wanadaiwa kutenda kosa hilo Novemba 25, 2024 katika eneo la Navy Wilaya ya Kigamboni; na kwa pamoja wanadaiwa kusafirisha kilo 424.77 za dawa za kulevya aina ya methamphetamine.
Shtaka la pili ni kusafirisha dawa za kuelvya aina heroine, tukio wanalodaiwa kulitenda Novemba 25, 2024 eneo la Navy Kigamboni, baada ya kukutwa na heroine zenye uzito wa kilo 22.53.