TABORA United inapiga hesabu ndefu juu ya namna gani itaikaribisha Simba nyumbani na papo hapo kocha wa timu hiyo ameshtukia kitu na fasta akaomba mechi mbili za kujipima nguvu haraka.
Tabora itafungua mwaka kwa kuikaribisha Simba katika mechi ya kiporo ya Ligi Kuu Bara itakayopigwa Februari 2 kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi, mjini Tabora huku timu hiyo ikiwa na kumbukumbu ya kupigwa mabao 3-0 zilipokutana katika mchezo wa kwanza Agosti mwaka jana.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha wa timu hiyo, Anicet Kiazayidi alisema programu yao ya maandalizi inakwenda sawa, lakini kabla ya kukutana na Simba amewasilisha maombi kwa uongozi wa klabu hiyo kumtafutia mechi mbili za kirafiki.
Kiazayidi alisema anaiheshimu Simba kuwa ni timu kubwa iliyotoka katika joto la mechi kubwa za kimataifa, hivyo anaamini mechi hizo mbili anazozitaka mapema kabla ya kukutana nao zitasaidia kuwapa ubora wachezaji kabla ya kukutana na vinara hao wa msimamo wa ligi.
“Tutakuwa na mchezo mgumu ujao, Simba ndio timu inayoongoza msimamo wa ligi hapa, lazima ujipange sawasawa namna ya kukutana nao, tunaendelea na mazoezi ila tunahitaji mechi mbili ya kujiandaa vyema ambazo naamini zitawarejesha moto wachezaji,” alisema Kiazayidi na kuongeza;
“Hawa wenzetu( Simba) msisahau wametoka katika mechi kubwa za mashindano ya Afrika na wamefanya vizuri lazima na sisi tujipange sawasawa haitakuwa mechi rahisi kwetu.”
Simba imefuzu robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika kwa kuongoza kundi.