Rais Samia amwapisha mganga mkuu akimpa maagizo kuhusu magonjwa ya milipuko

Dodoma. Rais Samia Suluhu Hassan amemuagiza Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Grace Magembe, kwenda kusimamia vyema magonjwa ya milipuko ili kuepusha nchi kuingizwa katika tahadhari (alert) na kusimamishwa kusafiri.

Agizo hilo linakuja ikiwa ni siku mbili baada ya Rais Samia kutangaza kubainika kwa mtu mmoja mwenye maambukizi ya Virusi vya Marburg (MVD) katika Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera huku akisema nchi imefanikiwa kuyadhibiti maambukizi hayo.

Rais Samia ametoa agizo hilo leo Jumatano Januari 22, 2025, Chamwino Ikulu, jijini Dodoma, wakati akiwaapisha majaji wanne wa Mahakama ya Rufani aliowateua Januari 10, 2025. Walioteuliwa ni pamoja na Jaji Latifa Alhinai Mansoor, George Masatu, Dk Deo Nangela, na Dk Ubena Agatho.

Aidha, Januari 17, 2025, Rais Samia alimteua Dk Grace Magembe kuwa Mganga Mkuu wa Serikali akichukua nafasi ya Profesa Tumaini Nagu ambaye uteuzi wake ulitenguliwa. Kabla ya uteuzi huo, Dk Magembe alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).

Akizungumza baada ya kuwaapisha, Rais Samia amewataka walioteuliwa kwenda kuwajibika vizuri mahali wanapopelekwa kutekeleza majukumu yao.

“Grace, umekuwa Mganga Mkuu wa Serikali, ni jukumu kubwa kweli kweli linalohitaji umakini kweli kweli. Sasa naomba haya mambo ya milipuko, milipuko yanayotokea katika nchi yetu uende ukasimamie vyema wewe na timu yako.

“Ni imani yangu kwamba utakwenda kuifanya kazi yako kama unavyotakiwa kuifanya na kuiepusha nchi yetu na kuingizwa na kutolewa kwenye alert (tahadhari) na kusimamishwa usafiri na mambo mengine kama hayo,” amesema huku akimsisitiza kuifanya kazi yake kwa umakini mkubwa.

Aidha, Rais Samia amewataka viongozi wengine walioapa wakawe mabadiliko kwenye maeneo waliyopelekwa na kufanya kazi vizuri ili matunda yaonekane.

“Tumefanya kazi vizuri, sasa hakuna muda wa kurudi nyuma, ni kwenda mbele, niwaombe sana kila mmoja alipopelekwa akasimamie wajibu wake,” amesema Rais Samia.

Wakati huohuo, Rais Samia amempongeza Kamishna wa Maadili wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Sivangiliwa Mwangesi kwa kulisha viapo kila anapoteua viongozi.

“Lakini sijui nimekunyima meno, sijasikia jaji kampa adhabu huyu normally (kawaida), ukiniletea aonywe, aelekezwe hebu kuwa na meno, siku moja niambie Rais huyu anyukuliwe, ndio watu watakaa sawa,” amesema Samia.

Akimkaribisha Rais Samia azungumze katika hafla hiyo, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amesema majaji wa rufani ni wazoefu mahakamani na pia wote waliokula viapo leo wamekuwepo serikalini, hivyo wanajua umuhimu wa kutunza viapo vyao.

“Ninapoendelea kukushukuru kwa kuendelea kuwawezesha Watanzania kupata nafasi zaidi ya kupata haki ambayo wanastahili, naomba sasa nikukaribishe uweze kuongea na wateule hawa na sisi wengine tupokee maelekezo lakini pia Watanzania wengine wakusikie,” amesema Dk Mpango.

Awali, Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Juma amesema uteuzi wa majaji hao umeongeza nguvu katika Mahakama ya Rufani kutoka majaji 35 hadi 39, nguvu ambayo inatafsiriwa ni ongezeko la majopo kutoka 11 hadi 12 ya majaji.

“Uwezeshaji huu umetuwezesha kupunguza mlundikano wa mashauri, utatusaidia sana sana kuondoa msongamano magerezani,” amesema Jaji Mkuu.

Amesema Novemba mwaka jana, alitembelewa na Kamishna wa Magereza nchini (CGP), Jeremia Katundu, ambaye alimweleza kuwa ongezeko la majaji wa rufani na Mahakama Kuu matokeo yake yanaonekana magerezani.

Kamishna huyo alimwambia uwezo wa kubeba mahabusu na wafungwa magerezani hadi Novemba mwaka jana ni 29,000, lakini hivi sasa wamepungua na kuna nafasi 2,000 za kujaza.

“Sio nafasi nzuri, lakini uwezo wao wa kuhudumia wafungwa na mahabusu wachache umekuwa ni mkubwa zaidi, kwa hiyo kuna nafasi ya maofisa magereza kufanya kazi nyingine zaidi ya ulinzi. Kazi yao (maofisa magereza) kubwa ni kurekebisha,” amesema Jaji Mkuu Juma.

Amesema matunda ya kuongeza majaji katika Mahakama hiyo ya Rufani hayaonekani kwa majaji tu, bali hata katika taasisi nyingine na kwenye uchumi.

“Alitupongeza sana katika kutumia teknolojia katika kusikiliza mashauri na alitoa ahadi kwako kuwa watatumia video conference kusikilizia rufani na akaomba na sisi Mahakama Rufani zote tuweze kusikiliza kwa video conference,” amesema.

Jaji Mkuu Juma amesema kutumika kwa teknolojia hiyo kunaleta unafuu zaidi kwa Jeshi la Magereza ikiwa sambamba na usalama kutokana na uwepo wa baadhi ya mahabusu na wafungwa ambao ni hatari kuwasafirisha kwa magari kutoka sehemu moja kwenda nyingine.

“Wakiwa na vifaa, rufaa zikasikilizwa pale pale inawaongezea uwezo wa kiusalama na inapunguza gharama,” amesema.

Related Posts