Upelelezi kesi ya wanaodaiwa kuchana noti za Sh4.6 milioni upo hatua za mwisho

Dar es Salaam. Upelelezi wa kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili washtakiwa 13, wakiwamo waliokuwa watumishi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), upo katika hatua za mwisho kukamilika.

Kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matano, likiwamo la kuharibu noti zenye thamani ya Sh4.6 milioni kwa kuzichanachana, hivyo kuisababishia benki hiyo hasara ya Sh4.6 bilioni.

Wakili wa Serikali, Winiwa Kasala ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, leo Jumatano Januari 22, 2025 wakati kesi hiyo ilipotajwa, akisema upelelezi upo katika  hatua za mwisho.

Washtakiwa katika kesi hiyo ya uhujumu ni Mariagoreth Kunzugala maarufu Bonge, Henry Mbowe maarufu Mzee wa Vichwa, Asha Sekiboko, Cecilia Mpande, Agripina Komba, Zubeda Mjewa, Khadija Kassunsumo na Mwanaheri Omary wote walikuwa wafanyakazi wa BoT na wakazi wa jijini Dar es Salaam.

Washtakiwa wengine ambao sio watumishi wa BoT ni Alistides Genand, Musa Chengula, Zaituni Chihipo na Respicius Rutabilwa.

Kasala ametoa taarifa hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Ana Magutu.

“Kesi hii imekuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake upo katika hatua za mwisho, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa,” amedia Wakili Kasala.

Hakimu Magutu baada ya kusikiliza maelezo hayo, alikubaliana na upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hadi Februari 20, 2025 kwa kutajwa.

Washtakiwa wapo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba Mahakama Kuu.

Katika hati ya mashtaka inadaiwa, kati ya Januari 2017 hadi Septemba 30, 2019, washtakiwa wakiwa watumishi wa BoT, kwa kuvunja majukumu yao ya kazi waliwezesha utendekaji wa kosa la kuongoza genge la uhalifu.

Pia, inadaiwa, Genand, Mchegage, Chengula, Chihipo na Ishengoma wakiwa si watumishi wa BoT, kwa kushirikiana na watumishi hao wa BoT kwa makusudi, waliwezesha kutendeka kosa la uhalifu wa kupanga.

Katika shitaka la tatu, washtakiwa wote bila ya kuwa na kibali na kutokuwa wazalendo, waliharibu noti za Sh10,000 kila moja kwa kuzikatakata zenye thamani ya Sh4.6 milioni.

Katika shitaka la nne, siku na maeneo hayo, kwa mawasilisho ya kilaghai, kwa kujua na kwa mpango wa kitapeli washitakiwa wote walijipatia faida ya Sh bilioni 1.5 kutoka BoT baada ya kuwasilisha noti hizo BoT.

Katika shitaka la tano washtakiwa wote wanadaiwa kuisababishia BoT hasara ya Sh4.6 milioni.

Awali, washtakiwa hao walikuwa wanakabiliwa na mashtaka sita, lakini Juni 18, 2021, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) Slyvester Mwakitalu aliwafutia shtaka la kutakatisha fedha, hivyo kubaki na mashtaka matano.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Decemba 14, 2020.

Related Posts