KIKOSI cha Simba kinajiandaa na mchezo wa hatua ya 64-Bora ya Kombe la Shirikisho la ndani dhidi ya Wonders ya Kilimanjaro utakaopigwa Jumapili hii kwenye Uwanja wa KMC Complex, huku kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids akiandaa mikakati mipya ya kukabiliana na wiki tatu ngumu.
Wiki hizo tatu ni za mshikemshike wa Ligi Kuu Bara ambao unatarajiwa kuanza kuanzia Februari 2, ambapo ‘Wekundu wa Msimbazi’ watakuwa na michezo sita na kati ya hiyo mitatu ni ya nyumbani na mingine ya ugenini.
Simba ilishinda mechi za raundi ya kwanza dhidi ya wapinzani wote itakaorudiana nao Februari kwa jumla ya mabao 14-0, ingawa jambo hilo halimfanyi Fadlu kubweteka na badala yake ameweka mikakati ya kuhakikisha hadondoshi pointi.
“Tunatambua haitakuwa rahisi kwa sababu ya ushindani na baadhi ya timu kufanya maboresho katika dirisha dogo la usajili lililopita, kitu pekee ambacho tunataka kukifanya ni kuhakikisha kila mchezo wetu tunauchukulia kwa usiriasi mkubwa.”
Kocha huyo ambaye ameipelekea Simba hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, alisema malengo yao ni kutwaa ubingwa baada ya kuukosa misimu mitatu.
“Kasi ya washindani wetu inatufanya pia kuongeza juhudi katika kila mchezo, tunatambua wazi gepu la pointi moja kwetu halitupi kujiamini katika kutimiza malengo hayo, jambo la muhimu ni kushinda michezo yetu bila ya kuangalia wengine wanafanya nini.”
Simba itaanza kushuka kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi Tabora Februari 2, kucheza dhidi ya Tabora United ambayo mechi ya mzunguko wa kwanza iliyopigwa KMC Complex Mwenge jijini Dar es Salaam, ilishinda mabao 3-0, Agosti 18, mwaka jana.
Baada ya hapo itasafiri hadi Babati mkoani Manyara kucheza na Fountain Gate Februari 6, ambayo pia mchezo wa raundi ya kwanza jijini Dar es Salaam ilishinda mabao 4-0, Agosti 25, mwaka jana, kisha kuwakaribisha Maafande wa Tanzania Prisons.
Mchezo huo na Prisons utapigwa Februari 11, ambapo Simba mechi ya kwanza ilishinda bao 1-0, Oktoba 22, mwaka jana, kisha baada ya hapo itaialika Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa KMC, ambayo iliichapa pia bao 1-0, Septemba 29, mwaka jana.
Kituo kinachofuata kwa Mnyama kitakuwa kwenye Uwanja wa Majaliwa Ruangwa kucheza na Namungo FC Februari 19, huku mechi ya kwanza zilipokutana Simba ilishinda mabao 3-0, Oktoba 25, mwaka jana, kisha kurejea Dar kucheza na Azam FC Februari 24, ambao mechi ya mwisho zilipokutana iliposhinda mabao 2-0 Zanzibar.