Ikanga Speed aomba mechi, aanza kusuka mipango

KIKOSI cha Yanga kinaendelea kujifua kwa ajili ya kurejea katika mechi za michuano ya ndani ikiwamo Ligi Kuu Bara na Kombe la Shirikisho baada ya kutolewa Ligi ya Mabingwa Afrika, huku winga mpya wa timu hiyo, Jonathan Ikangalombo ‘Ikanga Speed’ akiomba mechi hizo mapema.

Winga huyo aliyetua katika dirisha dogo kutoka AS Vita ya DR Congo anayemudu pia kucheza kama straika, ameanza kusuka mipango mipya baada ya kuishuhuduia timu hiyo iking’oka CAF na kusema anatamani kuanza kuitumikia timu hiyo hasa kwa alichokigundua kupitia mechi ya MC Alger ya Algeria.

Nyota huyo aliyeikamua Yanga mamilioni ya fedha katika usajili wake, akisainishwa mkataba wa miaka miwili, hakutumika katika mechi ya mwisho ya Yanga kwa vile alishaitumikia AS Vita katika mechi za awali za Kombe la Shirikisho Afrika na kibarua chake kipo katika mechi za mashindano ya ndani na amesema anatamani hata kesho kushuka uwanjani kuliamsha.

Yanga itarejea katika mechi za nyumbani wikiendi hii ikiikaribisha Copco ya Mwanza katika Kombe la Shirikisho kabla ya wiki ijayo kuipokea tena Kagera Sugar katika mchezo wa kiporo cha Ligi Kuu Bara utakaopigwa Februari Mosi, yote ikichezwa kwenye Uwanja wa KMC Complex, jijini Dar es Salaam.

Mechi hizo zinasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa Yanga kwa kutaka kuwaona nyota wawili wa timu hiyo akiwamo beki Israel Mwenda aliyesajiliwa pia dirisha dogo kutoka Singida Black Stars.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ikanga Speed, raia wa DR Congo alisema alikuwa jukwaani wakati Yanga iking’olewa CAF na kufunguka kwamba, ilikosa bahati tu kwenda robo fainali ya Ligi ya Mabingwa, ila anaamini itarudi kwa nguvu katika Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho ambako ndiko atakakoanza kuonyesha kile kilichoifanya ang’olewe AS Vita kuja Jangwani.

“Nilikuwa naumia wakati nikiwa jukwaani kwani, niliona nina kitu ambacho kingeisaidia timu yangu, lakini kwa vile kanuni zilikuwa zinanizuia, sasa naomba nipewe mechi hizi za michuano ya ndani tuitafute tiketi ya CAF kwa msimu ujao,” alisema Ikanga Speed

Winga huyo ameliambia Mwanaspoti, anasubiri mzunguko wa pili wa ligi kwa hamu kubwa ili aweze kuonyesha uwezo alionao.

“Nimekuja kwa ajili ya kufanya kazi na ninaamini nitaifanya vyema kwa kufuata maelekezo ya kocha wangu na kushirikiana na wachezaji wenzangu ili kufikia malengo ya timu msimu huu.”

Mapema kocha aliyewahi kufundisha Yanga na kumnoa Ikanga Speed, Raoul Shungu alinukuliwa akisema kuwa, Ikangalombo ni winga asilia wa kulia anayejua kutengeneza nafasi za mabao akiwa na kasi na akili ya kuwapenya mabeki wa timu pinzani.

Shungu alisema, mbali na kutengeneza nafasi pia Ikangalombo ana uwezo wa kufunga, ambapo akiwa Vita alitengeneza safu bora ya ushambuliaji akisaidiana na Elie Mpanzu kabla hajatimkia Simba.

Rekodi zinaonyesha katika mechi 12 ambazo AS Vita inayoongoza kundi lao la Ligi Kuu hakufanikiwa kucheza katika mechi sita za mwisho, lakini katika sita za mwanzo alifunga bao moja huku akitoa asisti mbili.

Mchezo wa mwisho kwa winga huyo kabla ya kutua Yanga ilikuwa Novemba 24 akicheza mechi ya dabi dhidi ya Renaissance, winga huyo akifunga bao pekee lililoipa timu yake ushindi ambapo pia akiibuka mchezaji bora wa mechi.

Faida kubwa ambayo Yanga wanakutana nayo ni kwa kuwa mchezaji huyo ana uwezo wa kutumika kwenye maeneo matatu tofauti eneo la mbele, winga wa kushoto, sehemu ambayo Yanga imekuwa na wachezaji tofauti tofauti, winga wa kulia na eneo la ushambuliaji wa kati ambalo Yanga pia imekuwa ikihaha kupata mchezaji sahihi.

Kutokana na Prince Dube na Kennedy Musonda kushindwa kufanya vizuri kwenye nafasi hiyo kwa msimu huu, huku Clement Mzize kwa upande wake anaonekana kufanya vizuri zaidi, mara kadhaa eneo la kushambulia kutokea kulia amekuwa akichezeshwa Pacome Zouzoua, lakini mawinga kiasili ndani ya Yanga ni Farid Mussa, Denis Nkane na Maxi Nzengeli.

Kati ya hao, Maxi ndiye mchezaji anayepata nafasi kubwa eneo hilo kuliko wenzake hao hivyo Ikangalombo nafasi yake inaonekana wazi katika wingi.

Related Posts