RIPOTI MAALUMU: Nyuma ya pazia anguko la viwanda Tanga

Kijana Bakari Rajabu (siyo jina halisi), mkazi wa Majengo jijini Tanga, anaishi maisha ya shida. Mahabusu na jela zimekuwa kama nyumbani kwake. Lakini, kwa maneno yake mwenyewe, hakupenda maisha haya.

“Nimelazimika kuingia katika uhalifu ili niishi. Ninaishia jela au mahabusu. Lakini watu hawaelewi. Mimi sipendi kuwa hivi,” anasema

Hata hivyo, Bakari, ambaye ndoto zake baada ya kumaliza shule ya sekondari zilikuwa kupata kazi, iwe ya ofisini au kiwandani, matumaini hayo yamefifia kutokana na ukosefu wa ajira.

Hadithi ya Bakari ni kielelezo cha mamia ya vijana jijini Tanga wanaokabiliana na tatizo la ukosefu wa ajira, changamoto ambayo inahusiana moja kwa moja na anguko la viwanda vilivyokuwa uti wa mgongo wa uchumi wa mkoa huu.

Bakari ni mmojawapo wa mamia ya vijana ambao wanakabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira na ni kielelezo halisi cha kudorora kwa viwanda katika jiji la Tanga, ambalo lilikuwa limejaa viwanda vilivyokuwa vinatoa ajira kwa vijana wengi.

Jengo chakavu la kiwanda cha Sikh Saw Mill, maarufu kwa kuchakata na kuzalisha mbao

Hadithi ya kudorora kwa miundombinu ya viwanda jijini Tanga ni kioo cha changamoto zinazoikumba sekta ya viwanda mkoani humo, huku athari zake zikidhihirika moja kwa moja katika maisha ya wananchi na uchumi wa serikali ya mkoa.

Tanga ya miaka ya baada ya Uhuru hadi mwanzoni mwa 2000 ilikuwa imechangamka. Ilikuwa na mamia ya wafanyakazi wa viwandani ambao siyo tu waliufanya mji huo kuwa na pilikapilika nyingi, bali kazi zao za uzalishaji zilisisimua uchumi wa mkoa huo na taifa kwa jumla.

Kulikuwa na viwanda kadhaa vilivyokuwapo Tanga wakati huo, lakini vitatu vilikuwa vikubwa na viliajiri mamia ya watu; Tanga Steel Rolling Mills kilikuwa kikizalisha bidhaa za chuma, zikiwemo nondo, mabati na vifaa vingine vya ujenzi.

Kilikuwapo kiwanda kingine kilichoitwa Sikh Saw Mill, maarufu kwa kuchakata mbao na kuzalisha samani, mbao za ujenzi na vifaa vingine vya matumizi ya viwandani na majumbani.

Kiwanda cha tatu kilikuwa cha mbolea, kilichojulikana kama Tanzania Fertilizer Company (TFC). Hiki kilikuwa na umuhimu mkubwa si kwa Tanga pekee, bali nchi nzima.

Viwanda hivyo havipo tena, vimekufa na hakuna hata dalili kwamba vitafufuka na kuendelea tena kusisimua uchumi wa Tanga. Majengo ya viwanda hivyo yametoweka kabisa na mengine yamegeuka kuwa magofu. Yapo yanayotumiwa na wachuuzi wa mitishamba.

Mtaalamu wa masuala ya uchumi kutoka Tanga, Kiama Mwaimu anaeleza kuhusu kifo cha viwanda hivyo, akibainisha kuwa kumeacha athari kubwa kiuchumi na kijamii kwa wakazi wake.

Kuhusu kiwanda cha chuma, anasema kilikuwa kikubwa kikizalisha nondo, mabati na vifaa vingine vya ujenzi ambavyo vilihitajika katika sekta ya ujenzi nchini, “kiwanda kilijulikana kwa kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu na kuchangia kupunguza utegemezi wa bidhaa za chuma kutoka nje ya nchi,” alieleza Mwaimu.

Kiwanda kiliajiri wafanyakazi zaidi ya 500 moja kwa moja. Hii ilijumuisha mafundi, wahandisi, na wafanyakazi wa kawaida, huku sekta nyingine zinazohusiana, kama usafirishaji na biashara ya malighafi, zikizalisha ajira zisizo za moja kwa moja.

Anasema kilianza kudorora mwishoni mwa miaka ya 1990 kutokana na sababu kadhaa ambazo zinaelezwa ni ushindani wa bidhaa za bei nafuu kutoka nje ambapo biashara za chuma kutoka nje, hasa Asia ziliathiri uwezo wa kiwanda kushindana sokoni.

Sababu nyingine ni gharama kubwa za uzalishaji, zikijumuisha umeme, upatikanaji wa malighafi kwa bei rahisi na changamoto za kiutawala, jambo lililoongeza gharama za uzalishaji.

Ofisa Biashara Mkoa wa Tanga, Peter Lyoko anasema kuanguka kwa Tanga Steel Rolling Mills kuliacha pengo kubwa katika sekta ya ujenzi na viwanda.

“Mapato ya kodi ya serikali yalipungua, wakazi waliopoteza ajira walikumbwa na hali ngumu ya kiuchumi na mzunguko wa fedha mkoani Tanga ulidorora,” anaeleza Lyoko.

Kiwanda cha Sikh Saw Mill kilikuwa maarufu kwa kuchakata mbao na kuzalisha samani, mbao za ujenzi na vifaa vingine vya matumizi ya viwandani na majumbani. Kiwanda hiki kilikuwa moja ya vyanzo vikubwa vya mbao za ubora wa juu nchini na kilihimiza maendeleo ya sekta ya misitu katika Mkoa wa Tanga.

Sikh Saw Mill kiliajiri mamia ya wafanyakazi moja kwa moja, ikiwemo mafundi seremala, wachakataji wa mbao na wafanyakazi wa kusafirisha bidhaa. Zaidi ya hapo, wakulima wadogo waliokuwa wakilima miti kwa ajili ya malighafi walinufaika kwa kuuza miti yao kwa kiwanda..

Mtaalamu mwingine wa uchumi, Dk Mzamil Kalokola, anaeleza kuwa sera dhaifu za uhifadhi wa mazingira, ikiwamo kutokuwepo kwa mipango thabiti ya usimamizi wa misitu ziliharakisha kuporomoka kwa sekta ya mbao.

Anasema sababu nyingine ni ushindani wa bidhaa mbadala. Kuongezeka kwa samani na vifaa vya mbao vya bei rahisi kutoka nchi za nje kulishusha mauzo ya bidhaa za kiwanda hicho.

Kuanguka kwa Sikh Saw Mill kuliathiri wakazi wa Tanga waliokitegemea kwa ajira ya moja kwa moja na kipato. Biashara za mbao na kilimo cha miti zilisambaratika, huku Serikali ikipoteza mapato ya kodi. Hali hii pia iliacha jamii ya karibu ikikabiliwa na changamoto za kiuchumi.

Kiwanda cha mbolea cha Tanga (TFC), kilikuwa moja ya viwanda muhimu katika ukanda wa Tanga na nchi nzima kwa jumla. Kiwanda hiki kilianzishwa miaka ya 1970, chini ya mpango wa Serikali wa kuimarisha sekta ya viwanda kama sehemu ya azma ya maendeleo ya uchumi wa taifa. Hata hivyo, mwishoni mwa miaka ya 1990, kiwanda hiki kilianza kudorora hadi kufungwa kabisa.

Dk Kalokola anasema sababu za kufa kwa kiwanda ni pamoja na ukosefu wa uwekezaji wa kutosha. Baada ya kuanzishwa, kiwanda hiki kilikumbwa na changamoto za uwekezaji wa kisasa, ikiwemo teknolojia ya kisasa ya uzalishaji. Serikali haikuweza kuwekeza vya kutosha kuboresha uzalishaji ili kushindana na mbolea ya bei nafuu kutoka nje.

Anasema katika kipindi hicho, kulikuwa na ongezeko la mbolea za bei nafuu zilizoingizwa kutoka nchi nyingine, jambo ambalo liliathiri soko la ndani. Bidhaa za kiwanda cha Tanga zilikuwa ghali kulinganisha na mbolea za nje.

Dk Kalokola pia anataja sababu za kiafya kuwa mojawapo ya kiwanda hicho kukosa mvuto. “Watu walikuwa wanakohoa sana inapotokea hitilafu inayosababishwa kuvuja kwa kemikali,” anasema Dk Kalokola, ambaye aliwahi kuwania uteuzi wa kuwa mgombea wa urais kupitia CCM.

Anasema hata hivyo, ubinafsishaji na usimamizi mbaya ni sababu kuu za kuanguka kwa viwanda hivyo: “Katika juhudi za kujaribu kubinafsisha viwanda vya umma, baadhi kama TFC vilitelekezwa au kushindwa kuendeshwa kwa ufanisi baada ya kuhamishwa kwa wawekezaji binafsi,” anasema mtaalamu huyo..

Kalokola anasema ukosefu wa malighafi pia umetajwa kuwa sababu ya kufa kwa kiwanda: TFC ilikuwa ikitegemea malighafi kutoka maeneo mbalimbali nchini na nje ya nchi. Hali ya miundombinu duni (hasa reli na barabara) ilifanya ugavi wa malighafi kuwa mgumu na wa gharama kubwa.

Wataalamu pia wanazungumzia kupungua kwa mahitaji ya mbolea ya ndani na changamoto katika sekta ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matumizi ya mbolea za viwandani na badala yake wakulima wengi kutegemea mbolea za asili (samadi na mboji) kuwa mojawapo ya sababu za kufa kwa TFC.

Kupotea kwa ajira kuliathiri mzunguko wa fedha, kwani kiwanda hicho kiliajiri mamia ya wafanyakazi wa moja kwa moja, pamoja na maelfu ya watu waliokuwa wakikitegemea kwa kazi za uzalishaji, usafirishaji na huduma nyingine za kiuchumi. Kufungwa kwake kulisababisha upotevu mkubwa wa ajira, hasa kwa watu wa kipato cha chini.

Pia Serikali ilipoteza mapato ya kodi kutoka kwa kiwanda hiki, ikiwa ni pamoja na ile ya bidhaa na ya wafanyakazi. Hali hii ilipunguza mchango wa kiwanda katika uchumi wa taifa na pia kuathiri uchumi wa Tanga ambapo kiwanda kilikuwa moja ya nguzo za kiuchumi katika Mkoa wa Tanga. “Pia kufungwa kwa TFC kulionekana kama pigo kwa juhudi za nchi kujenga viwanda kwa mujibu wa Sera ya Ujamaa na Kujitegemea iliyopo katika Azimio la Arusha ambalo lilisisitiza kuongeza thamani ya mazao ya kilimo ili kuongeza kipato cha wakulimu,” Dk Kalokola anasema.

Mkazi wa Tanga, Salma Hamisi anasema Tanga ilikuwa mkoa unaotegemewa sana kwa viwanda vyake. Tulitegemea viwanda kama Sikh Saw Mills na Tanga Steel Rolling Mills kutupatia ajira na kipato.

“Leo, vijana hawana kazi, na maisha yamekuwa magumu. Kufufua viwanda hivi kutarudisha matumaini kwa watu wa Tanga,” anaelezea.

Mfanyakazi wa zamani wa Sikh Saw Mills, Kassim Abdallah ambaye alifanya kazi kwa zaidi ya miaka 10, anasema kuwa kiwanda hicho kilikuwa mkombozi wa maisha ya familia yake.

“Tunahitaji viwanda kama hivi virejee ili kusaidia vizazi vya sasa na vijavyo,” anasisitiza umuhimu wa kiwanda hicho cha mbolea.

Naye mfanyakazi wa zamani wa Kiwanda cha Chuma, Said Salehe (75) anasema Serikali ilibinafsisha ikiwa haijajipanga na kama ilikuwa na mipango, basi haikuwa sahihi. “Ni sawa na mtu kuazima nguo yako halafu unamwachia aitumie kama anavyotaka yeye.

Anamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuleta viwanda Tanga ili watu wapate ajira. “Siyo sahihi kuwaita watu wa Tanga kuwa ni wavivu. Mbona viwanda vilipokuwa vinafanya kazi watu walikuwa wanakwenda kila siku kufanya kazi za vibarua?” aliuliza.

Alipoulizwa kama viwanda hivyo bado vinahitajika, alisema kuwa ni kweli vinahitaji, lakini akaitaka Serikali iangalie mahitaji ya sasa ili kujua ni viwanda gani vinaweza kufaa kwa Tanga.

Mkazi wa Makorora, Bakari Hoza anasema ukosefu wa viwanda ndio chanzo cha vikundi vya uhalifu vya vijana.

“Sidhani kama mtu ana kazi anaamka asubuhi anakwenda kazini atakuwa na fikra na nafasi ya kukaa afikirie kufanya mambo kama kuvuta bangi, kutumia madawa ya kulevya na kufanya uhalifu. Tunamwomba Mama aufufue mkoa. Sasa hivi Tanga imekufa ipoipo tu. Fursa hakuna. Leo ukipita Barabara ya Jamaa maduka yamefubaa, yamekufa kwa sababu hakuna biashara kutokana na watu kukosa uwezo wa kununua,” anasema Hoza.

Hamdan Hiza, mwenye umri wa miaka (80) ambaye alikuwa mfanyakazi wa TFC anakumbuka: “Tanga ilikuwa sehemu ya furaha tele. Viwanda viliwapa ajira na maisha bora. Lakini sasa hali ni tofauti kabisa, ajira hakuna na mzunguko wa fedha hakuna, tofauti na zamani.”

Mzee Abdallah Huseni (70), mkazi wa Mikanjuni aliyekuwa mfanyakazi wa Kiwanda cha Mbao, naye anasema kuanguka kwa viwanda hivi vitatu kulisababisha kupotea kwa nafasi nyingi za ajira, hali ambayo ilipunguza ustawi wa familia nyingi.

“Hali ya umaskini iliongezeka, vijana wengi waliokuwa wakitegemea viwanda hivyo walilazimika kuhamia maeneo mengine au kutafuta kazi zisizo rasmi,” anasema Huseni, akiongeza kuwa hali hiyo imeacha vilio na baadhi ya wafanyakazi bado wanaidai Serikali kutokana na kutolipwa maslahi yao.

Kushuka kwa Tanga Steel Rolling Mills na Sikh Saw Mill ni kielelezo cha changamoto ambazo viwanda vya ndani hukumbana nazo kutokana na mabadiliko ya kiuchumi, sera dhaifu na ushindani wa kimataifa.

Hatua za makusudi zinahitajika ili kufufua sekta ya viwanda Tanga kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji, kupunguza gharama za uzalishaji, na kuhimiza sera endelevu za uzalishaji. Kufanikisha hili kutasaidia kurudisha mzunguko wa kiuchumi na kuboresha maisha ya wakazi wa Tanga.

Usikose mwendelezo wa habari hii kesho ili kujua mikakati iliyopo ya kufufua shughuli za viwanda mkoani Tanga.

Related Posts