YANGA imeaga michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, lakini chapu kocha wa timu hiyo, Sead Ramovic ameanza msako wa kikosi kipya kwa msimu ujao, akianza kupigia hesabu beki wa Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini ili kuja kutengeneza ukuta wa maana.
Kama Yanga itamsajili beki huyo mpya, Sphiwe Given Msimango kinachofanya kazi pale nchini Afrika Kusini, itakuwa nafuu kwa mabeki waliopo sasa yaani Ibrahim Bacca na Dickon Job.
Kocha Ramovic mapema tu alishawaambia mabosi wake anahitaji beki wa kati mwenye makali ambaye atakuja kusaidiana na Bacca na nahodha msaidizi, Dickson Job wanaotumika mara kwa mara.
Taarifa kutoka ndani ya Yanga ni kwamba beki chaguo la kwanza kutoka kwa Ramovic ni kumshusha Msimango ambaye kwa sasa anaitumikia Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Kaizer inayofundishwa na kocha wa zamani wa Yanga, Nasreddine Nabi hamtumii sana beki huyo kwani katika mechi 12 za mashindano yote ilizocheza timu hiyo msimu huu, Msimango ametumika zisizozidi saba na kati ya hizo alizoanza hazizidi tatu, kwa vile mara nyingi anaingia ‘sub’.
Taarifa zinasema kuwa, Ramovic ameshazungumza na beki huyo ambaye amekubali kuungana naye Yanga mwisho wa msimu huu ambapo sasa hatua hiyo wameachiwa mabosi wa timu hiyo.
Msimango amewahi kufanya kazi na Ramovic alipokuwa TS Galaxy pia ya Afrika Kusini, lakini baadaye beki huyo anayecheza soka la ‘kazi ‘akauzwa Kaizer maarufu kwa jina la Amakhosi.
Ndani ya Kaizer mambo hayaonyeshi kumwendea sawa Msimango baada ya Nabi kuonyesha kuwaamini mabeki wengine nahodha Inacio Miguel raia wa Angola aliyesajiliwa na Mtunisia huyo anayecheza pamoja na mzawa Rushwin Dortley.
Hata hivyo, Yanga endapo itataka kumpata kwa haraka Masimango itahitajika kumnunua endapo Kaizer haitamuacha mwisho wa msimu kwa kuwa msimu huu ukimalizika beki huyo atabakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake.
Ramovic ameonyesha kuamini ubora wa Msimango kutokana na beki huyo pia anaweza kumudu kutumika kama kiungo mkabaji na akafanya vizuri.
Kama beki huyo atasajiliwa hatua hiyo itaendelea kuleta shaka kwa nahodha wa timu hiyo Bakari Mwamnyeto ambaye amekuwa akikosa mechi nyingi za timu hiyo akisotea benchi kisha kuingia katika mechi chache.
Msimango aliyezaliwa Mei 4,1997 ambaye mkataba wake na Kaizer utamalizika Juni 30, 2027, mbali na TS Galaxy na Kaizer, pia amewahi kukipiga Johannesburg na Highlands Park za Sauzi.