AKILI ZA KIJIWENI: Mpanzu atulize mawenge anajua mpira

USAJILI ambao Simba iliufanya wa kumsajili Elie Mpanzu katika dirisha dogo la usajili ulikuwa gumzo kubwa nchini kutokana na jina ambalo mchezaji huyo kutoka DR Congo alikuwa nalo kabla hata hajaja.

Ni jambo la kawaida kwa Watanzania kumpamba mtu hata kama hawajajiridhisha kwa kumtazama vya kutosha, wewe wape tu picha, maelezo wataandika wenyewe.

Sasa Mpanzu alipokuja hapa maskani kwetu tukakubaliana tumpe muda ili tujiridhishe kama mtu kweli au Simba wameuziwa mbuzi kwenye gunia tuanze kuwapa pole mapema kabla hata msimu haujachanganya.

Jamaa ndani ya muda mfupi aliocheza ameonyesha ana vitu muhimu vya kiufundi ambavyo mchezaji anatakiwa kuwa navyo kama vile ukokotaji wa mpira, kuupokea na kuuchezea pia ana uwezo wa kupasia.

Tatizo kubwa ambalo Mpanzu amelionyesha katika mechi ambazo ameichezea Simba hadi sasa ni kukosa utulivu na uamuzi sahihi pindi anapokuwa jirani na lango la timu pinzani kitu ambacho kinampunguzia sifa zake.

Anaweza kuwa na mpira sehemu ambako anatakiwa apige pasi yeye akalazimisha kupiga shuti na baadhi ya nyakati ambazo anatakiwa apige unaweza kuona akipasia mtu mwingine.

Pale anapoamua apige, mashuti yake mengi yamekuwa yakipaa, kutoka nje au kubabatiza wachezaji wa timu pinzani jambo ambalo linakuwa halina faida kwa timu na linainyima fursa ya kupata mabao mengi.

Ninachokiona kinampoza Mpanzu ni kupania kulikopitiliza hasa kwa kutaka kufunga bao hili kuwaziba midomo wale ambao wameanza kukosoa usajili wake, Simba imepigwa kwa vile hana bao hadi sasa na ana pasi moja ya mwisho.

Mpanzu anapaswa kuwa na utulivu na asipanie sana kwani hiyo ndiyo nzuri ya kujiweka katika mazingira mazuri kisaikolojia yatakayoipa timu fursa ya kunufaika na ubora wake jambo ambalo baadaye litampa heshima yeye mwenyewe.

Related Posts