JAMBO lililotukosha hapa kijiweni ni kipa Feruzi Teru aliyekuwa chaguo la tano pale Simba kujiunga na Kagera Sugar dirisha dogo.
Kilichotufurahisha ni mdogo wetu kupata ufahamu kuwa alikuwa anapoteza muda na kipaji chake pale Simba kwani nafasi ya kucheza isingekuwa rahisi kupatikana kwake.
Fikiria bila kumhesabu Ayoub Lakred, Feruzi mbele yake kulikuwa na makipa wanne ambao alipaswa kuonyesha kiwango bora zaidi yao ili apate nafasi ya kucheza.
Kuna makipa watatu wa timu za taifa ambao ni Moussa Camara wa Guinea ambaye nyuma yake kuna Aishi Manula na Ally Salim wa Taifa Stars wakati huo kuna kipa mwingine wa nne, Abel Hussein ambaye ni mzoefu kuzidi Feruzi Teru.
Ni tofauti na Kagera Sugar ambako mtihani mkubwa anaoenda kukabiliana nao ni wa kumtoa langoni Ramadhan Chalamanda ambaye ndiye kipa chaguo la kwanza na mmoja wa manahodha wa Kagera Sugar.
Feruzi ana uwezekano wa kucheza pale kwa vile Kagera Sugar imekuwa na utamaduni wa kutoa nafasi kwa makipa wao tofauti na chaguo la kwanza kumbuka msimu uliopita, Said Kipao na Allan Ngereka wote walicheza.
Jambo la muhimu kwa Feruzi ni kuhakikisha anafuata nyayo za Hassan Dilunga ambaye kipindi fulani aliwahi kupata fursa ya kuichezea Yanga iliyokuwa imesheheni hivyo hakuwa akipata nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Dilunga alichukua uamuzi mgumu wa kuacha posho na mishahara minono aliyokuwa akilipwa Simba na kutimkia Mtibwa Sugar kwa lengo la kusaka nafasi ya kutosha ya kucheza.
Uamuzi wake ulilipa kwani alifanya vizuri akiwa na Mtibwa Sugar hadi akasajiliwa kwa fedha nyingi na Simba na baadaye akawa miongoni mwa mastaa wakubwa.