Mwanza. Halmashauri ya Wilaya ya Magu mkoani Mwanza imepanda miti 633,000 katika kipindi cha Julai hadi Desemba 30, 2024 ikiwa ni nusu ya malengo yake ya kupanda miti 1,500,000 waliyopangiwa na Serikali katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Hayo yameelezwa Januari 22, 2025 na Ofisa Maliasili na Uhifadhi wa Mazingira Wilaya ya Magu, Ngussa Buyamba wakati wa hafla ya kupokea na kupanda miche 8,000 ya miti katika Shule ya Wasichana ya Mwanza Sekondari.
Miche hicho imetolewa na Taasisi ya Via Aviation inayojishughulisha na masuala ya usafirishaji wa anga ambayo imeanzisha kampeni ya kupanda mti kwa kila mteja anayehudumiwa katika taasisi hiyo.
Amesema miche hiyo 633,000, imepandwa tangu kuanza kwa mwaka 2024/25 huku akisema halmashauri imepokea miche mingine 100,000 kutoka kwa wadau mbalimbali ambayo itapandwa kwa awamu tofauti kufikisha jumla ya miti iliyopandwa hadi sasa kufikia 738,000.
Ametaja changamoto za kimazingira zinazoikumba wilaya hiyo kuwa ni pamoja na ukataji holela wa miti kwa ajili ya matumizi ya nyumbani ikiwemo kupikia, matumizi mabaya ya ardhi na uvunaji holela wa misitu.
Kutokana na changamoto hizo, ofisa huyo amesema zimeanzishwa sheria ndogo ngazi ya halmashauri na vijiji sambamba na kuhuisha kamati za udhibiti rasilimali kwenye vijiji huku wakiweka adhabu kali kwa waharibifu wa misitu.
“Tumeihuisha sheria ndogo mwaka 2023 kudhibiti ukataji miti ambapo atakayekata miti bila kibali atatozwa faini ya Sh50,000 hadi 300,000 na kulazimishwa kupanda miti mingine.
“Vijiji 10 vyenye changamoto ya ukataji miti hovyo vina sheria ndogo za kutoza faini ya Sh50,000 na kupitia sheria hizo atakayekutwa na hatia anashughulikiwa,” amesema Buyamba.
Ofisa huyo ameeleza awali, vijiji hivyo havikuwa na mpango wa matumizi bora ya ardhi, hivyo walianzisha mpango huo ambapo vijiji 22 kati ya 82 wilayani humo vinautekeleza huku ukisaidia kuepusha ukataji hovyo wa miti.
“Tunatoa elimu na kuhamasisha miradi ya utunzaji vitalu vya miche, kupanda miti, na tayari bustani tatu za miche zinazozalisha wastani wa miche 360,000 kila mwaka na tunahamasisha upandaji miti ya matunda ili kuboresha lishe na uhifadhi,” amesema.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Taasisi ya Via Aviation, Susan Mashibe, uamuzi wa kugawa miche hicho wilayani Magu umechangiwa na uwepo wa athari za kimazingira zinazochangiwa na shughuli za usafirishaji wa anga zinazoendeshwa na taasisi hiyo.
Pia, amesema taasisi hiyo kupitia mpango huo unaolenga kurejesha kwa jamii utawezesha upandaji wa miti 1,000,000 nchi nzima ikiwemo ya matunda ili kuongeza usalama wa chakula na uchumi wa jamii za Kanda ya Ziwa na kwa kuanza wameanza na miche 100,000.
“Usafirishaji wa anga unachangia kuchafua mazingira hivyo tunahamasika kutunza mazingira kwa kuotesha miche ya kutosha, tumeanza na Magu kwa kuwapa miche 100,000 na lengo letu ni kurudisha mazingira kwenye asili yake,” amesema Susan.
Kwa upande wake, Katibu Tawala Wilaya ya Magu mkoani humo, Jubilate Lawuo amesema miche hiyo siyo tu itasaidia kurejesha uoto wa wilaya hiyo, pia itaboresha ustawi wa jamii kwa kuongeza kivuli na usalama wa chakula.
“Hapa Magu kulikuwa na changamoto kubwa ya ukataji miti mpaka unashtuka lakini tukaja na huo mkakati wa kuandaa miche. Tunahakikisha tunafuatilia hii miti tunayoikabidhi na kuipanda ili istawi na miti iliyobaki tutaendelea kuisambaza katika taasisi zetu,” amesema Lawuo.
Ili kuhakikisha mpango huo unakuwa endelevu, miche hiyo imekabidhiwa kwa Shule ya Sekondari ya Wasichana Mwanza takriban 633.
Mwanafunzi katika shule hiyo, Rehema Haji amesema shule hiyo iluyoanzishwa mwaka 2023, inapitia changamoto ya ukosefu wa kivuli hata hivyo kukabifhiwa miche hiyo imerejesha matumaini kwake baada ya kupandwa.
”Miti hii itatusaidia kupata matunda na kupendezesha mazingira kwa sababu shule yetu ni mpya kunakuwa na upepo, kwahiyo tutaitunza na kuiwekea mbolea ili kuhifadhi mazingira ya shule yetu,” amesema Rehema.
Miche 100,000 iliyokabidhiwa na kupandwa wilayani humo, inajumuisha miche ya miti ya matunda, mbao na vivuli.