Boni Yai asimulia jinsi Mbowe alivyoyapokea matokeo, vilio VIP

Dar es Salaam. Baada ya ukimya wa saa kadhaa, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu Boni Yai amesema matokeo ya jana Jumatano, Januari 22, 2025 ya uchaguzi wa chama hicho yaliwamwaga machozi baadhi ya makada.

Amesema pamoja na vilio vya baadhi ya makada wa chama hicho waliokuwa wanamuunga mkono Freeman Mbowe, mwenyewe hakuwa katika hali hiyo.

Jacob anaeleza hayo baada ya ukimya wa saa kadhaa tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa chama hicho uliompa ushindi Tundu Lissu kuwa mwenyekiti wa Chadema.

Mbowe aliyekuwa mwenyekiti wa miaka 21 amejikuta akiwekwa kando na wajumbe wa mkutano mkuu uliohitimishwa jana Jumatano katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.

Mbali na Mbowe na Lissu kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi huo alikuwamo pia Charles Odero.

Katika uchaguzi huo uliofanyika, Januari 21 na kukamilika jana Januari 22, 2025, Lissu ameshinda kwa kura 513 dhidi ya 482 alizopata Mbowe, huku Odero akiambulia kura moja.

Kupitia ukurasa wake wa X, leo Alhamisi Januari 23, 2025, Jacob ambaye alikuwa wakala wa Mbowe kwenye kuhesabu kura, ameandika baada ya mchakato wa kuhesabu kura, alikwenda kumjulisha Mbowe matokeo halisi.

“Nilipokujulisha matokeo ya uchaguzi kuwa wajumbe 482 walihitaji uwe Mwenyekiti wao na wajumbe 513 wameamua ukapumzike, watu wengine uliokuwa nao chumba cha VIP wakiwa wanalia wewe ulinyanyuka ukanikumbatia.

“Kisha ukachukua simu yako ili kupongeza na kukubali matokeo kupitia ukurasa wako wa X na kuanza kujadili suala la kurudi ukumbini tayari kupokea matokeo rasmi,” amesema.

Sambamba na hilo, amemtaja Mbowe hakuwa kiongozi tu kwake, bali ni mwalimu, mwanafalsafa, mkufunzi, mzazi, mlezi na rafiki wa kweli.

“Nashukuru kwa kuniamini na kunipa jukumu la kuwa mwenyekiti wa kampeni zako katika uchaguzi mkuu wa chama Januari 2025.

“Unajua, umeona, umesikia na umeshuhudia hadi sekunde ya mwisho nilivyosimama na wewe na nilivyojitoa kwa hali na mali kufanya jukumu lile zito lililokuwa mbele yetu lakini bahati haikuwa upande wetu,” ameandika.

Amesema hakuwahi kufikiri au kudhani ipo siku Mbowe angempa nafasi ya kusimamia kazi yake ya siasa.

“Hata hivyo nachezwa na machale, ninavyokufahamu itakuwa ulikuwa kuna kitu ulitaka nijifunze kwenye majukumu yangu ya kusimamia kampeni zako,” amesema.

Amesema kwa hatua hiyo, amejifunza mambo mengi na kwamba hatasahau daima.

“Sitasahau pale uliponiambia, watu wako rasmi uliowapa jukumu la kufanya kampeni wasifanye jambo lolote bila idhini yako na pia katika kila jambo tutakalofanya tusikiumize chama kwa namna yoyote ile au kwa kisingizio chochote kile,” amesema.

Amesema mapenzi ya Mbowe kwa Chadema na wanachama wake ndiyo sababu ya yeye kuridhia kubeba jukumu la kumfanyia kiongozi huyo kampeni.

“Ulistahili ushirikiano wangu hata kama dunia nzima ingekusaliti kisiasa na kukugeuka bado mimi ningebakia peke yangu kuwa pembeni yako,” ameandika.

Kwa sababu hiyo, amesema alipoona kura hazijatosha hakuhitaji ruhusa yake kusaini fomu ya matokeo kuwa Lissu ni mshindi.

“Wewe utabakia kuwa jenerali wangu wa kweli na kiongozi wangu siku zote. Nitakuwa tayari siku yoyote na mahala popote kutumwa au kupokea majukumu kutoka kwako hata nje ya siasa,” amesema.

Alichokiandika Mbowe kwenye ukurasa wake wa X kabla ya matokeo kutangazwa akisema: “Nimepokea kwa mikono miwili maamuzi ya uchaguzi wa mkutano mkuu wa chama chetu Chadema uliohitimishwa leo asubuhi 22 Januari 2025. Nampongeza Mhe. Tundu Lissu na wenzake kwa kuaminiwa kutwikwa jukumu la Uongozi wa Chama. Nawatakia kila la kheri katika kukipeleka mbele Chama chetu.”

Related Posts