KOCHA Mkuu wa Namungo, Juma Mgunda ametaja mambo yatakayombeba kwenye mechi 14 za duru la pili zilizobaki ili kuihakikishia timu hiyo kucheza Ligi Kuu msimu ujao.
Namungo ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo baada ya kucheza mechi 16 ikikusanya pointi 17, imeshinda mechi tano, sare mbili na vipigo tisa na kwenye mechi hizo imefunga mabao 11 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 19.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mgunda ambaye ni mzoefu wa ligi ya Tanzania, alisema ana kazi kubwa ya kuhakikisha anairudisha Namungo kwenye ushindani huku akiweka wazi ni kuwajenga kisaikolojia wachezaji, kurudisha morali na mbinu zitakazompa matokeo kwenye mechi zilizo mbele yake.
“Sio rahisi lakini nina imani kubwa nitaisaidia Namungo kurudi kwenye ushindani kwa kufanya mambo hayo, naamini wachezaji watarudisha timu sehemu nzuri baada ya kushindwa kufanya hivyo mzunguko wa kwanza,” alisema na kuongeza;
“Wachezaji waliopo Namungo wote wamepevuka, wanaelewa namna ya kufanya ili kuiweka timu kwenye ushindani, hivyo ili waweze kufanya hivyo muhimu ni kuwajenga kisaikolojia na kuwarudisha kwenye morali,” alisema.
Mgunda alisema mabadiliko yaliyofanya dirisha dogo kwa kupunguza na kuongeza wachezaji anaamini yatakuwa na chachu kikosini na kila kitu kitakwenda kama alivyopanga;
“Nina imani na wachezaji waliobaki na walioongezwa kwa sababu ni mapendekezo tangu.”
“Uongozi umefanya kazi yake kwa kusajili wachezaji ambao kwa asilimia kubwa ni mapendekezo yangu, sasa kazi imebaki upande wangu na wachezaji kuhakikisha tunafanya kile kinachotarajiwa na wana Mtwara kuona timu hii inaendelea kucheza ligi kuu msimu ujao,” alisema.
Mechi tano za Namungo baada ya kurejea kwa ligi ni dhidi ya Tabora United ugenini, Dodoma Jiji nyumbani, Tanzania Prisons ugenini, Simba na Coastal Union nyumbani.