Dodoma. Unaweza ukawa ni mvutano mpya kuhusu Katiba kati ya Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), baada ya Makamu Mwenyekiti wa CCM-Bara, Stephen Wasira, kusema kuwa hoja ya kutaka mabadiliko ya Katiba kabla ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025 imechelewa.
Wasira ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Januari 23, 2025 jijini Dodoma katika hafla ya mapokezi katika makao makuu ya chama hicho, ikilenga matamshi ya Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, ambaye alisema, “hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi.”
Akizungumza na wajumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa chama hicho, Lissu alisisitiza kuwa mabadiliko ya Katiba ni lazima kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mvutano huu unaonyesha changamoto zinazozikumba juhudi za kutafuta maridhiano ya kitaifa, huku uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ukikaribia.
Lissu, alisema Chadema inakubaliana na wazo la maridhiano, lakini kwa sharti kuwa yatakuwa na mwelekeo chanya.
Alisema: “Kama hakuna Katiba mpya, basi hakuna uchaguzi.”
Wasira amesema CCM iko tayari kwa mazungumzo na chama chochote kwa lengo la kufanikisha maridhiano.
Hata hivyo, ameongeza kuwa baadhi ya madai ya Chadema yanahitaji muda mrefu, hasa suala la Katiba mpya.
“Chadema walileta mambo 11 mezani. Katika awamu ya kwanza ya mazungumzo, mambo sita yalijadiliwa na manne yalifikiwa mwafaka. Lakini mabadiliko ya Katiba ni jambo nyeti na hayawezi kufanikishwa ndani ya muda mfupi.
“Leo ni Januari, Bunge linaisha Juni, na litakuwa ni Bunge la Bajeti. Huo muda wa kujadili Katiba mpya utatoka wapi?” amehoji Wasira.
Wasira pia alikosoa kauli mbiu ya Chadema ya “No reforms, no election,” akisema ni amri badala ya pendekezo. “Hiyo ni amri, sio pendekezo. Mazungumzo hayawezi kufanikiwa kwa kauli kama hizo,” amesisitiza.
Pamoja na tofauti zao, Wasira amesisitiza kuwa CCM inatilia mkazo maridhiano na iko tayari kushirikiana na wadau wote, wakiwemo wa vyama vya siasa, mashirika ya kidini na asasi za kiraia.
Amesema: “Tutazungumza na kila mmoja ili tupate amani na kuleta maendeleo.”
Amesema kila sheria ni lazima ipitie bungeni na kwamba, mchakato wake ni mrefu, huku akieleza kuwa muda wa uhai wa Bunge la sasa umebaki mdogo kabla ya kuvunjwa.
Akizungumza mbele ya umati wa wanachama wa CCM na vongozi waliofika kumpokea ikiwa ni mara yake ya kwanza kuingia ofisini tangu alipochaguliwa na Mkutano Mkuu Maalumu wa CCM wa Januari 18, 2025, ni kama alikuwa anatupa jiwe kwa Chadema.
Hata hivyo mwenyewe alisisitiza: “Hapa simsemi mtu yeyote, lakini kuna mtu alikuwa anasema na mtambue hivyo. Kwenda kwenye uchaguzi unaposema lazima kwanza tutunge sheria wakati Bunge linavunjwa Juni au Julai, hivi hawajui kuwa ni mchakato kufikia hatua hiyo?.”
Kwa mujibu wa Wasira, CCM kimefungua milango yake kwa ajili ya mazungumzo na maridhiano kwa namna ambavyo vyama vinaweza kuingia kwenye uchaguzi huku akisisitiza kuwa hilo linawezakana hata kama hakuna sheria zilizobadilishwa.
“Tuko tayari kuzungumza kuhusu tunawezaje kuingia kwenye uchaguzi ili twende pamoja, waje sasa tuzungumze maana tunajua faida ya kufanya mazungumzo,” amesema Wasira.
Akizungumzia namna watakavyoingia kwenye uchaguzi wa mwaka huu wakiwa na matumaini ya kushinda, Wasira amesema mpaka sasa wana mtaji wa wanachama 12.5 milioni sawa na asilimia 40 ya wapigakura.
Kuhusu migogoro ya ardhi ameagiza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kupitia upya mikataba yote ya watu wanaomiliki ardhi na ikigundulika kuna watu wamepewa kinyume na sheria, wanyang’anywe haraka.
Ameseme sheria za nchi zinampa mamlaka Rais kusaini kwa ajili ya kuruhusu ardhi ichukuliwe na mtu mwingine, lakini kama kuna mahali imefanyika kinyume na hapo, basi waliopewa watambue kuwa wamepewa kinyemelea na wanastahiri kuirudisha mikononi mwa umma.
Naye Spika mstaafu, Job Ndugai amemwomba Wasira kupeleka salamu za wananchi wa Mkoa wa Dodoma kwamba watahakikisha mkoa huo unaongoza kwa kutoa kura nyingi za Rais kwenye uchaguzi utakaofanyika mwishoni mwa mwaka huu.
Ndugai ambaye ni Mbunge wa Kongwa, amesema kupitia Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, Alhaj Adam Kimbisa wameshaseti mitambo na sasa kinachosubiriwa ni muda ili waweze kufanya kwa vitendo.