Dar es Salaam. Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amebainisha kwamba jiji hilo liko mbioni kuanza kufanya shughuli za kiuchumi ikiwemo biashara na kazi mbalimbali kwa saa 24.
Kwa tafsiri ya mkuu huyo wa mkoa sasa Dar es Salaam kutakuwa hakuna kulala kwa wafanyabiashara huku akisema ni tija kwa vijana hasa wasio na ajira katika kujiingizia kipato.
Ameyasema hayo leo Januari 23, 2025 kwenye hafla ya utoaji Tuzo kwa Walipa Kodi bora wa mwaka 2023/24 ya Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyofanyikia katika Ukumbi wa The Super Dom Masaki jijini Dar es Salaam iliyohudhuriwa na Rais Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba na Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson.
“Mkoa wetu kwa kushirikiana na taasisi zote za Serikali tumejipanga kuanza biashara saa 24 lengo kubwa ni kuwaweka vijana katika sekta hizo zisizo rasmi vijana ambao hawana ajira pamoja na kupanua wigo wa huduma kwa mkoa wetu.
“Mabasi yanafanya kazi saa 24 na mara nyingi kumekuwa kunakosekana mnyororo wa thamani wa namna ya mtu anaweza kupata huduma katika maeneo mbalimbali jijini hapa,” amesema Chalamila.
Amesema hatua inayofuata sasa ni kufunga kamera wakianza na soko la Kariakoo ambazo kwa sasa zimeshaagizwa.