Yanga yaficha wawili wapya | Mwanaspoti

KATIKA usajili wa dirisha dogo uliofungwa Januari 15 mwaka huu, Yanga ilitambulisha wachezaji wawili pekee ambao ni beki Israel Mwenda kutoka Singida Black Stars na Jonathan Ikangalombo anayemudu kuicheza winga zote mbili na mshambuliaji akitokea AS Vita ya DR Congo.

Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya Yanga zinabainisha kuna majembe mengine mawili yamemalizana na klabu hiyo ndani ya kipindi hicho cha usajili.

Wanaotajwa kumalizana na Yanga huku wakiwa wamefichwa na klabu hiyo wote wanatokea Zanzibar ambao ni mshambuliaji wa Mlandege, Abdallah Idd Mtumwa ‘Pina’ na kiungo Khleffin Salum Hamdoun aliyewahi kuitumikia Azam.

Mtoa taarifa huyo ambaye ni mtu wa karibu na Pina, amebainisha usajili wa mshambuliaji huyo uliingiliwa na Pamba Jiji ambayo nayo ilikuwa ikimpigia hesabu za kumsajili wakati wa dirisha dogo.

Chanzo hicho kilifichua kipindi cha michuano ya Kombe la Mapinduzi 2025 ikiendelea Kisiwani Pemba, ndipo viongozi wa Yanga walikwenda kukamilisha dili hilo wakati mshambuliaji huyo akiitumikia Zanzibar Heroes iliyobeba ubingwa.

“Ni kweli Pina amesaini mkataba wa kuitumikia Yanga, pia kulikuwa na mazungumzo baina yake na Pamba Jiji ambayo pia inaelezwa mchezaji na timu hiyo walifikia makubaliano na kusaini mkataba wenye thamani ya Sh40 milioni,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza.

“Baada ya kukaa mezani na timu zote mbili tulifikia uamuzi wa kurejesha fedha ya Pamba Jiji na kuhusu Yanga tulikubaliana nao kuwa ataitumikia timu hiyo kuanzia msimu ujao kutokana na kuchelewa kumuingiza kwenye mfumo wa usajili baada ya sakata la kumwaga wino timu mbili kwa wakati mmoja.”

Kwa upande wa Khleffin Salum Hamdoun ambaye inaelezwa jina lake liliingizwa kwenye mfumo wa usajili dirisha dogo lililofungwa Januari 15 mwaka huu, ametokea Muscat Club

ya Oman aliyokuwa akiitumikia tangu mwaka 2022.

Khleffin ambaye ni kiungo mshambuliaji, kabla ya kwenda Oman alikuwa akiitumikia Azam ambao ilimsainisha mkataba wa miaka minne Januari 2020 akitokea Mlandege na mkataba wake huo ulifikia kikomo Desemba 2024.

Related Posts