Maagizo ya Rais Samia TRA, wakwepa kodi moto waja

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amewataka watendaji na watumishi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka mazingira ya kuchochea rushwa na ukwepaji kodi.

Amesema mtumishi yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo visivyofaa kwa maendeleo ya nchi hana budi kufuatiliwa na kushughulikiwa.

Ameagiza uongozi wa mamlaka hiyo kufuatilia mienendo hiyo na kuchukua hatua haraka kwa watumishi wachache wanaotengeneza mazingira ya kutokuwa na usawa wa ulipaji wa kodi nchini.

Rais Samia ametoa kauli hiyo usiku wa jana Alhamisi Januari 23, 2025 kwenye hafla ya utoaji Tuzo kwa Walipa Kodi bora wa mwaka 2023/24 ya Mamalaka ya Mapato Tanzania (TRA) iliyofanyika kwenye Ukumbi wa The Super Dom Masaki jijini Dar es Salaam.

“Pamoja na mifumo tunayoiweka, lazima mfanye kazi kwa uadilifu ili kuleta na kudumisha mafanikio yaliyopo na kuleta mengine zaidi. Kamishna mkuu lazima usimamie usawa katika ulipaji wa kodi nchini,” amesema Rais Samia.

Rais Samia amesema hatua zichukuliwe haraka bila upendeleo  kwa mtumishi yeyote anayejihusisha na vitendo hivyo vinavyoikosesha nchi haki.

Akizungumzia madhara ya ukwepaji kodi amesema inaathiri wananchi, wafanyabiashara na nchi kwa ujumla kwani inachelewesha maendeleo ya Serikali kwa kushidwa kutekeleza mipango yake kwa wakati.

“Kuzorotesha utoaji huduma za kijamii ikiwemo kuchelewesha madawati na dawa kwenye vituo vya afya, usambazaji wa umeme kwa makazi na viwanda,” amesema.

Amewataka watendaji kusimamia usawa katika ulipaji wa kodi huku akisema sio suala linalofaa pale ambapo mtu mmoja analipa huku mwingne halipi na kwamba sio haki.

Amesema ni lazima uchumi uendele kukua ili Serikali ipate kodi na wale wote wanaolipa kodi kwa wakati na hiyari amewapongeza.

Kuhusu utendaji wa mamlaka hiyo, ameipongeza kutoka na ukusanyaji wake wa mapato ambapo kwa mwaka wa fedha uliopita ilifanikiwa kukusanya Sh16 trilioni kati ya Sh30.4 trilioni walizopangiwa ikiwa ni sawa na asilimia 54 ya kiasi wanachotakiwa kukusanya mwaka huu wa fedha.

Amesema kwa mwenendo huo ni wazi TRA inaweza kukusanya kiasi cha Sh4 trilioni kwa mwezi. Amesema hilo linatokana na kuimarishwa kwa mifumo ya ndani ya TRA pamoja na kubadili mitindo ya utendaji kazi pia kutanuka kwa wigo wa walipakodi watokanao na uwekezaji na wazalishaji.

“Tunataka mfumo wa kodi utakaorahisisha mfumo wa kiuchumi na kukua kwa mapato ya ndani unaweza kukataa msaada wa mtu kwakuwa unaweza kujiamiani,” amesema.

Pia amesema TRA lazima iepuke kutoza kodi zisizostahiki kodi ya dhuluma yani pale mtu alipe zaidi.

Aidha ameowaomba wafanyabiashara waendelee kulipa kodi na waepuke kukwepa wala kutengeneza mazingira yasiyokubalika.

Amesema malengo ya Serikali ni kupunguze utegemezi wa kibajeti kama inavyosema ilani ya CCM kwa mfano kwa mwaka huu wa fedha bajeti ni Sh49.3 trilioni ambapo Sh30.4 trilioni zinararajiwa kutokana na mapato ya kodi.

Amesema ndio maana amekuwa akisisitiza mifumo ya taasisi za kiserikali zisomane kurahisishsa biashara kuziba mianya ya upotevu wa mapato na kurahisisha biashara.

Amesema mwelekeo wetu lazima uwe kuongeza idadi ya walipa kodi. Lazima tuweke sera na mikakati sekta isiyo rasmi iwe rasmi

Aidha Rais Samia amepongeza tuzo hizo kwa kuchochea ulipaji kodi huku akisema mwakani tuzo hizo zitakuwa za Rais.

Awali, Kamishna Mkuu wa TRA, Yusuph Mwenda amesema malengo ya mamlaka hayo ni kukusanya kodi ili siku moja Tanzania ijitegemee yenyewe kwa mapato yake ya ndani.

Katika kufanikisha hilo amesema kama mamlaka wanaendelea kuimarisha mazingira ya ulipaji kodi kwa kuimarisha mahusiano na walipakodi nchini pamoja na kuboresha mazingira ya mfumo wa ulipaji kodi.

“Tutajitahidi kukusanya kodi kwa kiwango kikubwa bila migogoro na walipaji, kusimamia maadili kwa watumishi wa TRA, kutatua migogoro na kusimamia ulipaji kodi wa hiyari, kupunguza cash economy kwenye nchi yetu,” amesema Mwenda.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya TRA, Mussa Uledi amesema wamekuwa wakifanyia kazi maelekezo yote wanayopewa na Rais Samia na miongoni mwa maelekezo hayo ni kuhakikisha mifumo ya TRA na taasisi nyingine inasomana na katika hilo wameanza kutumia mfumo wa TANCIS unaorahisisha utendaji kazi bandarini, mipakani na katika viwanja vya ndege.

Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema kauli ya Rais Samia kutaka kodi ikusanywe kwa hiari imezaa matunda kwa kupatikana kwa makusanyo makubwa ya Kodi pia Rais ameunda Tume ya kufanya mapitio ya Sheria za Kodi na pia kuiwezesha TRA kujenga mifumo inayoweza kuleta tija kwenye makusanyo.

Dk Mwigulu amesema katika kipindi hiki cha Rais Samia ameongeza kwa kiasi kikubwa fedha katika sekta ya kilimo, huduma za jamii, sekta ya afya na katika miundombinu ambapo barabara zinajengwa mijini na vijijini.

Related Posts