Mambo manne yalivyoibeba Ligi Kuu Bara

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imesema kupanda kwa viwango vya ubora wa Ligi Kuu Bara kumetokana na mambo makuu manne.

Kwa mujibu wa Shirikisho la Kimataifa la Historia na Takwimu za Mpira wa Miguu (IFFHS), Ligi Kuu Bara imekuwa ya nne kwa ubora barani Afrika na ya 57 duniani kwa mwaka 2024 ikikusanya pointi 266.75.

Ligi hiyo inayoshirikisha timu 16, imepanda kwa nafasi mbili kutoka ya sita mwaka 2023 hadi ya nne 2024 ikizipiku Ligi za Afrika Kusini na Tunisia.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ofisa Habari wa Bodi ya Ligi, Karim Boimanda, amesema katika mambo yaliyoibeba zaidi ligi hiyo huwezi kuwaweka kando wadau.

Mbali na wadau, Boimanda ameutaja uwekezaji mkubwa uliofanywa ndani ya ligi, usimamizi imara kutoka Bodi ya Ligi na namna ambavyo Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilivyoimarisha ulinzi na kuifanya ligi kuchezwa sehemu salama na yenye amani.

“Yanapotoka matokeo kama haya inaonyesha kuna shughuli fulani imefanyika na imetoa matokeo chanya. Haya yamekuja kutokana na kilichofanywa na wadau wote wa ligi kila mmoja kwa nafasi yake amefanya kitu cha maendeleo. Wadau unaweza kuzizungumzia klabu kutokana na kufanya usajili bora, pia imeajiri maofisa bora wa ufundi.

“Unapotengeneza kikosi bora basi inahitaji usimamizi bora, kwa hiyo Bodi ya Ligi imefanya usimamizi bora wa ligi ambao tumekuja kushuhudia ushindani na matokeo ya haki uwanjani.

“Msingi wa yote hayo inabaki palepale kwamba klabu inahitaji fedha, pia ligi inahitaji fedha ili iweze kuendelea ndiyo maana kuna wadhamini ambao wamefanya kazi kubwa sana kwenye maendeleo haya tunayozungumza leo. Wadhamini wakuu wa ligi ambao ni Benki ya Biashara, mdhamini mwenye haki za matangazo ya video kwa maana ya Azam Media na TBC ambao ni mdhamini mwenye haki za matangazo ya redio. Wote hao kila mmoja ametimiza majukumu yake vizuri.

“Lakini tunayazungumza yote hayo kutokana na Tanzania ni nchi yenye amani, hii ni ishara kwamba Serikali imekuwa ikitutengenezea mazingira rafiki ya sisi kusimamia na kuendesha ligi, kwa hiyo hatuwezi kutaja wadau waliochangia kwa kiasi kikubwa matokeo chanya haya bila ya kuitaja Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Mazuri yote hayo tumeyazungumza lazima yawafikie watu, yanawafikiaje, hapo unawahusisha wanahabari, kwa hiyo wao wamekuwa kama nahodha wa hii kampeni, tunafanya vitu vingi vizuri lakini mwisho wa siku tunawahitaji wao kuitangazia dunia tunachokifanya.

“Mimi naamini waandishi wa habari wamefanya kazi kubwa na ya kipekee ndiyo sababu tumekuwa maarufu na kupanda juu, wamekuwa watu muhimu sana katika kuitangaza ligi yetu,” alisema Boimanda.

Orodha ya ligi kumi bora Afrika kwa mujibu wa IFFHS ipo hivi; Misri (pointi 694.5), Morocco (pointi 459.5), Algeria (pointi 347), Tanzania (pointi 266.75), Tunisia (pointi 263), Afrika Kusini (pointi 262.75), Angola (pointi pointi 261), DR Congo (203.75), Nigeria (pointi 201) na Botswana (pointi 170.75).

Related Posts