Makocha wa timu nne zinazoshika mkia kwenye msimamo wa ligi kuu Tanzania Bara wana wiki mbili za kujiandaa kujibu mitihani miwili migumu ambayo inaweza kuzifanya mbili zishuke daraja moja kwa moja mwishoni mwa msimu.
Vizingiti hivyo viwili ni ubutu wa safu za ushambuliaji na pia kushindwa kuzimudu mechi za ugenini.
Udhaifu katika kufunga mabao na pia kupata matokeo mazuri kwa mechi za ugenini, kumechangia kwa kiasi kikubwa kuzifanya timu hizo nne kuwa katika nafasi mbaya ambazo zipo sasa kwenye msimamo wa ligi.
Makocha Amani Josiah wa Tanzania Prisons iliyo nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi na Felix Minziro ambaye timu yake Pamba Jiji FC inashika nafasi ya 14 ndio wana kazi kubwa ya kufanya kuhakikisha timu zao zinarudi zikiwa na makali kwenye safu zao za ushambuliaji.
Timu hizo kila moja imefunga mabao saba katika mechi 16 zilizopita ikiwa ni wastani wa bao 0.4 kwa mechi.
Na usajili ambao timu hizo zimeufanya katika dirisha dogo lililopita la usajili, unaashiria shabaha ya Tanzania Prisons na Pamba Jiji kutamani kutorudi kinyonge katika upande wa kushambulia.
Wachezaji saba wa nafasi za ushambuliaji wamesajiliwa na Pamba Jiji katika dirisha dogo huku Tanzania Prisons ikisajili washambuliaji watatu.
Kagera Sugar imefunga mabao 10 katika mechi 15 ikiwa ni wastani wa bao 0.7 kwa mchezo na katika dirisha dogo ilimnasa kiungo mmoja mshambuliaji na KenGold iliyofunga maba0 11 katika mechi 11 sawa na wastani wa bao 0.7 iliimarisha kikosi chake kwa kuwanasa wachezaji saba wa nafasi za ushambuliaji.
Kutafuta dawa ya kumaliza unyonge ugenini ni kibarua kingine kinachowakabili makocha wa timu hizo nne hasa wa KenGold, Vladislav Heric.
KenGold ndio timu ambayo hadi sasa haijapata pointi hata moja ugenini ambapo imepoteza zote tisa huku Kagera Sugar ikipata pointi mbili tu katika michezo saba ambayo haikuwa nyumbani.
Tanzania Prisons imekusanya pointi nne ugenini katika mechi nane na Pamba Jiji FC kati ya pointi 27 ambazo ilitakiwa kupata ugenini, imevuna pointi tano tu.
Kocha wa Tanzania Prisons, Amani Josiah alisema kuwa anaamini timu yake itarudi kivingine ligi ikirejea.
“Nimewaambia wachezaji wangu kusahau yaliyopita na tupambane na hizi mechi ambazo ziko mbele yetu kwa vile hizo tulizopoteza zimeshaondoka,” alisema Josiah.
Kocha wa Pamba Jiji FC, Felix Minziro alisema kuwa mkakati wao ni kuanza vizuri ligi ikirejea.
“Tunahitajika kukusanya pointi nyingi katika mechi tano za kwanza ligi ikirudi. Hizo zitatuweka katika fursa nzuri ya kusogea juu kwenye msimamo,” alisema Minziro.