Dar/mikoani. Hospitali za mikoa na kanda nchini zimekiri kupokea mgonjwa mmoja mpaka wawili kila siku waliopata madhara ya shinikizo la juu la damu, baada ya kuishi na ugonjwa huo kwa muda mrefu bila wao kujua au kusitisha matibabu. Madhara yaliyotajwa kuwapata ghafla, ni pamoja na kiharusi (kupooza/‘stroke’), mshtuko au shambulizi la moyo, moyo kushindwa kufanya kazi na ugonjwa sugu wa figo unaosababisha figo kushindwa kufanya kazi. Kwa mujibu wa madaktari, hilo ni ongezeko la miaka ya hivi karibuni ikilinganishwa na zamani ambapo walipokea wastani wa mgonjwa mmoja au wawili kwa wiki au mwezi.
Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Benjamin Mkapa, Edwin Ochina anasema: “Jana (juzi) Januari 22 tumepokea wagonjwa watatu waliopata madhara ya shinikizo la juu la damu kwa kupata kiharusi na kwao ni hali iliyowakuta ghafla. Tunapokea wagonjwa wawili mpaka watatu kwa siku. Kuna wakati unawapata mpaka wanne kwa siku na hii inatufanya tunaweza kuwa na wagonjwa watano mpaka 10 kwa wiki waliopata madhara ya shinikizo la juu la damu,” anasema.
Dk Ochina anasema mara nyingi wagonjwa hao hufika wakiwa wamepata kiharusi, mshtuko au shambulio la moyo, lakini wanaongoza zaidi kupata kiharusi.
“Wengi wanapata kiharusi, kwa mwezi wanaopata shambulio la moyo unaweza kukuta mmoja na ambaye figo zimefeli mmoja. Lakini pia wengine figo inaweza kuumia na mgonjwa asionyeshe dalili za haraka, lakini tunaona mkojo unatoka kidogo na akifanyiwa uchunguzi tunabaini na wengine wanapata presha ya macho,” anasema Dk Ochina.
Ukubwa wa tatizo hili unaonyeshwa kupitia takwimu za Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete, ambako kwa wagonjwa 100,025 waliofika kupata matibabu, asilimia 52 walibainika kuwa na shinikizo la damu.
Daktari bingwa wa magonjwa ya moyo JKCI, Tulizo Shemu anafichua kuwa kati ya watu wazima 10, watatu mpaka watano nchini Tanzania wana shinikizo la juu la damu na zaidi ya asilimia 60 hawajitambui.
“Ugonjwa huu madhara yake ni makubwa, unasababisha watu kupata kiharusi, figo kushindwa kufanya kazi, mshtuko na vifo vya ghafla, kupumua kwa shida na kuvimba miguu, macho kutoona, kifafa cha mimba na kupoteza ujauzito,” anasema Dk Tulizo.
Kwa mujibu takwimu za Wizara ya Afya, kuanzia Julai 2023 hadi Machi 2024 magonjwa yaliyoongoza kwa wagonjwa wa nje (OPD) wenye umri chini ya miaka mitano, shinikizo la juu la damu liliathiri kundi hilo kwa asilimia 5.9, sawa na wagonjwa 737,730.
Wataalamu wa afya wanasema baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakipoteza maisha na wengine kupata madhara ya kudumu, hasa kwa wale wanaochelewa kupata huduma.
Frank Oswald (47) ni miongoni mwa wagonjwa waliopata kiharusi ghafla akiwa kazini baada ya kuishi kwa muda mrefu na shinikizo la damu bila kutambua.
“Nilianguka ghafla nikiwa kazini (Dar es Salaam), bahati nzuri, miongoni mwa wafanyakazi yupo aliyebaini hali iliyonikuta akashauri niwahishwe MOI (Taasisi ya Mifupa Muhimbili), ndani ya dakika 30 nilifika na moja kwa moja nilipelekwa chumba cha upasuaji,” anasimulia.
Frank anasema licha ya kwamba ilimchukua muda kupona, wataalamu wa afya walimweleza angechelewa asingerudi katika hali yake ya kawaida.
Anaeleza kuwa nyakati nyingi alisikia kichwa kuuma, moyo kwenda mbio, lakini alichukua jukumu la kupumzika au kumeza dawa za maumivu.
“Sikuwahi kuhudhuria hospitali kama miaka mitatu hivi, hivyo sikupata nafasi ya kupimwa shinikizo la juu la damu. Madaktari waliniambia nilikaa na presha kwa miaka mingi.”
Frank ni miongoni mwa makumi ya wagonjwa wanaopata madhara ya shinikizo la juu la damu kila siku nchini, ambao hata hivyo hawakuwahi kuwa na taarifa juu ya hali zao kiafya.
Hospitali za mikoa na kanda zimesema, Watanzania wengi hawana uelewa juu ya hali za afya zao, hivyo wengi huishi na shinikizo la juu la damu kwa muda mrefu wakitibu dalili, na mwisho huishia kupata madhara ya kudumu.
Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Morogoro imekuwa ikipokea mgonjwa mmoja mpaka wawili kwa siku wanaofika na madhara ya ugonjwa huo.
Akifanya mahojiano hospitalini hapo, Daktari bingwa wa magonjwa ya ndani na Mkuu wa Idara ya Magonjwa hospitalini hapo, Dk Kessy Ngarawa anasema wanapokea wagonjwa waliopata kiharusi baada ya kukaa na shinikizo kwa muda mrefu na wengine kutofuata maelekezo ya tiba.
“Kiharusi kilichotokana na shinikizo la damu lisilotibiwa kwa sasa imekua tatizo, wanakuja hawawezi kuongea kabisa na wameshachelewa. Tunapokea mmoja au wawili kila siku, kwa wiki watano mpaka sita wanaweza kupokelewa hapa hospitali.
“Wakifika tunaangalia ni aina gani ya kiharusi, kama mishipa imepasuka huyo anahitaji matibabu zaidi tunampeleka MOI na wengine tunawapeleka kwenye idara ya viungo,” anasema.
Dk Kessy anasema inatokea kwa wachache wanaobahatika kuwahi kufika na wakipata matibabu wanapona na kurudi kawaida.
Anasema baada ya tiba hiyo wamekuwa wakiwafikisha kliniki kwa ajili ya mwendelezo wa tiba zao.
Hata hivyo, anasema wapo wanaopokelewa na madhara ya shinikizo la juu la damu lakini hawakupata kiharusi. Hawa ni wengi na wanakuja wakiwa wamepoteza fahamu na presha iko juu. “Hawezi kutembea bila msaada na mwingine ameshapoteza kabisa fahamu hata macho hawezi kufungua.
“Mwingine anafika na shida ya upumuaji na mwingine figo haziwezi tena kufanya kazi, mara nyingi hawa huwa tunawalaza na kuwaanzishia vipimo ambavyo tunavifanya kwa CT Scan na Digital XRay inatusaidia sisi kugundua mapema tatizo.”
Hata hivyo, Dk Kessy anasema walio wengi hufika hospitalini hapo kwa rufaa, na kwamba baadhi yao wanakuwa na changamoto ya kuacha dawa. “Wapo wanaokuja na kubainika tayari walishakuwa na presha huko nyuma na magonjwa mbalimbali, matumizi ya dawa yakawa siyo sahihi, wameacha au hawatumii kwa usahihi. Wapo ambao walikuwa hawajui kabisa kama wana shinikizo la damu, wengine wanafika mpaka sukari haipimiki kabisa ipo zaidi ya 28 au 29,” anasema.
Kauli hiyo inaungwa mkono na Daktari wa magonjwa ya ndani katika kitengo cha moyo kutoka Hospitali ya Bugando, Mwanza, Fredrick Mugisha Kalokola anayesema idadi imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Hali hiyo anaitafsiri kama kukosekana kwa huduma maeneo ya pembezoni na watu kutokuwa na mwamko wa upimaji afya.
“Tunawaona wagonjwa wanaongezeka, wanaofika na shinikizo la damu wanaongezeka, lakini pia wanaofika kupima kwa hiari nao wanaongezeka, lakini wanaogundulika na kuletwa katika hali mbaya pia wanaongezeka kila siku tunawapokea,” anasema Dk Kalokola, ambaye pia ni Mkufunzi wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Afya shirikishi Bugando.
Dk Kessy anasema kinachochangia zaidi, Watanzania wengi hawana utamaduni wa kufanya uchunguzi wa afya na hiyo inachangia kuongeza gharama za matibabu na kuyumbisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na familia. “Kikubwa ambacho kinachangia hatuna utamaduni wa kufanya ‘check up’, si lazima uonane na daktari bingwa, lakini angalau mara mbili kwa mwaka nenda kachunguze uwezo wa macho yako kuona, sukari yako ikoje, nikijisikia tofauti naenda kituo cha afya kuona changamoto ni nini.
“Kufanya vipimo ni muhimu ili kujua hali yako, mtu anayepata madhara ya shinikizo la damu angeanza mapema kuna baadhi ya hali mgonjwa akiwa nayo, unaweza kumpa ushauri zaidi mapema,” anasema Dk Kessy. Takwimu za idadi ya wagonjwa 70,000 waliopimwa na kambi maalumu ya madaktari wa Samia katika kipindi cha Mei mpaka Julai 2024 katika halmashauri 184, asilimia 34 ya wagonjwa walioonwa walikuwa na shinikizo la juu la damu.
Akitoa ripoti hiyo Agosti 7, 2024, aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema;
“Shinikizo la juu la damu ni magonjwa yaliyoongoza kwa asilimia 34, hii ni salamu kwetu. Itabidi tufanye uchambuzi kwa maana ripoti ya hivi karibuni ilituonyesha asilimia 26 ya Watanzania, huku imeongezeka, wataalamu wanaingia kuchunguza tutaona tupo asilimia ngapi ikifika Desemba,” alisema Ummy.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete, Dk Peter Kisenge anaiambia Mwananchi wagonjwa wanaofuata huduma katika vituo va afya idadi ya wenye shinikizo ni kubwa ikilinganishwa na katika jamii.
“Tunapoenda kwenye jamii tunaona takwimu kama hizo, kwa JKCI hapa asilimia 30 ya wagonjwa tunaowaona wana shinikizo la juu la damu na kwenye kambi tukiwafuata mitaani tunawapata asilimia 26,” anasema.
Dk Kisenge, ambaye pia ni bingwa wa magonjwa ya moyo ameshauri jamii kubadili mtindo wa maisha, akisema asilimia kubwa ya watu hawafanyi mazoezi, huku wakiwa na ulaji mbaya, unywaji pombe uliokithiri, uvutaji sigara uliokithiri na kuwa na unene kupita kiasi, vitu vinavyochangia tatizo hilo.
Meneja wa Mpango wa Taifa wa kuzuia na kudhibiti magonjwa yasiyoambukiza kutoka Wizara ya Afya, Dk Omary Ubuguyu anasema tatizo walio wengi kwenye jamii hawajui kuhusu hali za afya zao. Anasema wagonjwa hao wapo hospitali, kwenye jamii na walio hospitali kuna taarifa mbili tofauti, waliopo kwenye jamii wapo wanaojijua na wapo wasiojijua.
Anasema takwimu zinaonyesha wanaohudhuria vituo vya afya wameongezeka kutoka wagonjwa wa shinikizo la damu 1,112,704 mwaka 2019 hadi 1,482,911 mwaka 2023.
“Tunafanya tafiti, ikiwemo ile ya Steps Survey, tunachagua maeneo maalumu na nyumba. Mwaka 2012 tafiti zilionesha watu 100 kati ya 26 walikuwa na shinikizo la juu la damu, sawa na kila watu wanne mmoja ana shinikizo la damu,” anasema.
Anasema tafiti zinaonesha kati ya hao, ni watu 700,000 tu waliotibiwa hospitalini.