Kampuni ya Puma Energy Tanzania, imeshinda tuzo nne wakati wa usiku wa utoaji tuzo kwa wafanyabiashara waliofanya vizuri kwa mwaka wa fedha 2023/24!
Tukio hili la kipekee lilifanyika wakati wa Usiku wa Hafla ya Utoaji Tuzo kwa Walipakodi lililofanyika katika ukumbi wa the Super Dome Masaki, Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Viongozi wa kiserikali, wakiwemo: Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Tulia Ackson (Mb), Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Nchemba (Mb), Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb), Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Bw. Emmanuel Tutuba, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA Tanzania) Bw. Yusuph Juma Mwenda, pamoja na viongozi wengine waandamizi wa serikali na dini walikuwepo pia kushuhudia wakati taasisi na biashara zaidi ya 100 zikitunukiwa na kutambuliwa kwa weledi wao.
Ikiwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Puma Energy Tanzania, Bi. Fatma Abdallah, kampuni hiyo kinara katika usambazaji na uuzaji wa huduma na bidhaa za mafuta na nishati imejinyakulia tuzo katika vipengele vya weledi wa ulipaji kodi katika sekta ya Uuzaji na Usambazaji wa Mafuta na Gesi kwa mwaka wa fedha 2023/24, kampuni bora zaidi iliyozingatia sheria katika ulipaji wa kodi ngazi ya kitaifa kwa mwaka wa fedha wa 2023/24, kampuni bora katika ulipaji wa wakati wa Kodi na Ushuru, na mshindi wa jumla katika ulipaji Kodi na Forodha uliolipwa katika Mwaka wa Fedha wa 2023/24 kwenye sekta ya Ushuru na Forodha.
Puma Energy Tanzania imeishukuru serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa heshima hii na ushirikiano katika shughuli mbalimbali za maendeleo ya kijamii na kiuchumi ili kusukuma mbele guruduma la maendeleo ya taifa.