EXIM Bank, Msalaba Mwekundu wapanda miti, wachangisha damu

 

BENKI ya Exim imeshirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) pamoja na Mpango wa Damu Salama Tanzania (NTBS) kupanda miti na kuendesha zoezi la uchangiaji damu katika maadhimisho ya Siku ya Msalaba Mwekundu Duniani. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Maadhimisho hayo yaliyofanyika jijini Dodoma ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Dk. Dotto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.

“Benki ya Exim tumejumuika pamoja hapa Dodoma kukumbuka na kuthamini kazi nzuri na ya muhimu inayofanywa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania (TRCS) kwa sababu tunatambua umuhimu wa kazi zake katika kusaidia jamii yetu, na tunaahidi kuendelea kuwa mshirika mwaminifu katika kuleta mabadiliko chanya,” anasema Stanley Kafu, Mkuu wa Kitengo cha Masoko kutoka Exim Bank.

Kupitia mpango wake wa kijamii unaoitwa ‘EXIM Cares’, Exim Bank ina miradi kadhaa ya kijamii na kimaendeleo ambayo imekuwa ikitekelezwa nchini Tanzania. Baadhi ya miradi hiyo ya benki ni katika sekta za afya, elimu, mazingira, ubunifu, na masuala ya kifedha.

Akielezea moja ya miradi hiyo, Stanley alisema, “Kupitia mradi wetu wa ‘EXIM Go Green’ tumeshirikiana na wadau kuiunga mkono serikali kutunza mazingira kwa kupanda miti. Mfano tumeshiriki kupanda miti katika kata ya Zuzu iliyopo hapa Dodoma tukiongozwa na Mizengo Pinda, Waziri Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Pia benki yetu imeshiriki kupanda miti katika Hospitali ya Rufaa ya hapa Dodoma na soko la Machinga Complex.”

Kwa upande wa afya, Benki ya Exim imekuwa ikishirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania pamoja na  Mpango wa Damu Salama Tanzania (NTBS) kusaidia katika zoezi la uchangiaji damu ikitambua umuhimu na uhitaji wake kwa Watanzania.

“Mwaka jana tulishirikiana na Mpango wa Damu Salama Tanzania (NTBS) kuratibu zoezi la uchangiaji damu katika mikoa ya Mbeya, Mtwara, Mwanza, Dar es Salaam na hapa Dodoma ambapo tulitambuliwa na Serikali kama moja ya wadau wakuu katika zoezi la uchangiaji damu hapa nchini,” anafafanua Stanley.

Mwaka huu, Benki ya Exim imeendelea kushirikiana na Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania katika maadhimisho hayo yenye kaulimbiu ya “Natoa kwa furaha, na furaha ninayotoa ni zawadi.” ikisisitiza umuhimu wa kujitoa ajili ya afya njema kwa wenye mahitaji na furaha inayoambatana na kitendo hicho kwa pande zote mbili kwa mtoaji na mpokeaji.

Related Posts