Dar es Salaam. Ushirikishwaji wa wadau wa nishati safi kuzalisha umeme umetajwa kuwa suluhisho la kukatika umeme mara kwa mara, linalokwaza uzalishaji viwandani na kwa wajasiriamali.
Miongoni mwa rasilimali za uzalishaji wa nishati zilizopo nchini ni gesi asilia, ambapo Tanzania ina futi za ujazo 57.54 na kati ya hizo, futi za ujazo trilioni 47.4 zimegunduliwa eneo la kina kirefu cha bahari na trilioni 10.12 nchi kavu.
Akizungumza jana wadau wa nishati na wamiliki wa viwanda jijini Dar es Salaam Januari 24, Naibu Meneja Msaidizi wa Kampuni ya Clarke Energy, Tarak Jani amesema changamoto ya kukatika kwa umeme inarudisha nyuma uchumi wa nchi, hivyo juhudi za pamoja kati ya Serikali na wadau zinapaswa kuunganishwa ili kupata suluhisho.
“Changamoto ya Tanzania si uzalishaji wa umeme, bali ni usambazaji wake wa uhakika. Viwanda vingi, vinapata hasara kwa kukosa umeme na hivyo kupunguza ufanisi wa uzalishaj,” amesema.
Amesema kampuni hiyo imewezesha kukuza uzalishaji wa viwandani kupitia teknolojia za kisasa na huduma za kiufundi za kuimarisha mfumo wa nishati nchini.
“Kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Shirika la Umeme (Tanesco) Clarke Energy inalenga kukuza usambazaji wa gesi asilia ili kuhakikisha viwanda vinaweza kutumia nishati safi, rafiki kwa mazingira, badala ya makaa ya mawe au vyanzo vingine vinavyotoa gesi chafu.
Ameongeza kuwa kampuni hiyo pia inatoa elimu kwa wateja wao juu ya matumizi bora ya gesi asilia na mbinu za kupunguza uzalishaji wa hewa ya ukaa kwa kutumia mifumo ya kupoza kama maji au mvuke.
Tunalenga kuchukua hatua madhubuti katika kuimarisha sekta ya nishati nchini Tanzania kwa kushirikiana na mashirika makubwa kama Tanesco na TPDC, ili kuhakikisha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa viwanda, taasisi, na jamii.
Meneja Mkuu wa Clarke Energy, Emile Hamman, amesema kwamba kampuni hiyo inaweka kipaumbele kwa kuimarisha sekta ya nishati kwa kushirikiana na Serikali.
“Clarke Energy haina miradi ya moja kwa moja ya uwekezaji katika uzalishaji wa nishati, lakini inatoa vifaa vya kuzalisha umeme na huduma za kitaalamu kwa wateja. Kwa mfano kituo cha Somanga, kilichopo mkoani Lindi, ni mojawapo ya maeneo ambako tumewezesha uzalishaji wa nishati kwa kutumia gesi asilia,” amesema.
Amesema kwa sasa kampuni hiyo ina mpango wa kupanua huduma zake katika mikoa yenye viwanda ikiwemo Dar es Salaam, Morogoro na Arusha, huku ikishirikiana na TPDC kuboresha usambazaji wa gesi.
“Kwa kuongeza idadi ya wazalishaji wa viwandani wanaotumia nishati safi, unaamini tutaongeza ufanisi wa kiuchumi na kuchangia maendeleo ya nchi.
Hamman ameongeza kuwa kampuni hiyo inaendeshwa na Watanzania katika nyanja mbalimbali, kuanzia uongozi wa juu hadi huduma za kiufundi, jambo linalodhihirisha kujitolea kwa Clarke Energy katika maendeleo ya ndani ya nchi.