Chilunda aja na akili mpya ya kazi

MSHAMBULIAJI wa zamani wa Simba, Shaaban Chilunda amesema baada ya kufanikiwa kusajiliwa na KMC kwa sasa ana akili mpya ya kufanya kazi ili kurudi katika ushindani baada ya kukaa nje ya uwanja kwa muda mrefu huku akisisitiza kwamba yupo tayari kwa ajili mapambano.

Chilunda aliwahi kuichezea timu hiyo kwa mkopo Januari, mwaka jana akitokea Simba aliyomalizana nayo mwishoni mwa msimu uliopita na kuwa mchezaji huru, jambo ambalo liliufanya uongozi kuanza hesabu za kumpata moja kwa moja kikosini.

Akizungumza na Mwanaspoti, mchezaji huyo alisema anawaheshimu wachezaji wote waliopo ndani ya kikosi cha KMC, lakini anaamini kuongezwa kwake anahitajika kuonyesha na kuongeza ubora eneo la ushambuliaji la timu hiyo.

“Ni kweli nilikuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu, nimerejea nikiwa fiti baada ya kufanya mazoezi kwa muda na kurejea katika utimamu nawahakikishia wana KMC kuwa nitapambana kuisaidia timu yetu iweze kufikia malengo,” alisema nyota huyo wa zamani wa Azam.

“Haitakuwa rahisi lakini kwa sababu ushindani umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka kwa timu na timu hivyo hivyo hadi kwa wachezaji natarajia changamoto kubwa, lakini hilo haliwezi kuniondoa kwenye malengo yangu.”

Chilunda alisema matamanio yake ni kurudi kwenye nafasi yake kwa ubora, hivyo atapambana kuhakikisha anatumia vyema kila nafasi atakayopewa kuitumikia KMC ambayo mchezo wake wa kwanza inatarajia kuanza dhidi ya Azam.

Related Posts