Huyu ndiye Gardner G Habash ‘Kapteni’ wa Jahazi la Clouds

Dar es Salaam. Mtangazaji wa kipindi cha Jahazi kinachorushwa na kituo cha redio cha Clouds FM, Gardner G. Habash amefariki dunia alfajiri ya leo Aprili 20, 2024 katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) alikokuwa akipatiwa matibabu.

Gardner ambaye ni baba mzazi wa msanii wa Bongofleva, Malkia Karen, hadi anaugua alikuwa bado anatangaza kipindi cha Jahazi akiwa na wenzake wawili—Musa Hussein na George Bantu.

Gardner ni mtangazaji wa pili kufariki dunia akiwa anakitumikia kipindi cha Jahazi, baada ya Ephraim Kibonde aliyefariki dunia Aprili 2021 akiwa anatibiwa katika Hospitali ya Bugando, mkoani Mwanza.

Katika maisha yake, Gardner alianza utangazaji wa redio akiwa Clouds FM, kisha aliondoka na kujiunga na Times FM alikotangaza kipindi cha Masikani.

Safari yake ya utangazaji iliendelea alipohamia E FM na kuanzisha kipindi cha Ubaoni, kabla ya kurejea Clouds FM mwaka 2016.

Mkurugenzi wa E FM, Francis Ciza ‘Majizzo’ kupitia ukurasa wake wa Instagram ameeleza kusikitishwa na kifo cha Gardner akisema wanatambua na kunathamini mchango wake kwenye tasnia ya habari.

“Kwenye miaka 10 ya E FM kuna mchango wake mkubwa wakati ule akiendesha kipindi cha Ubaoni. Bwana alitoa, Bwana ametwaa jina lake lihimidiwe. Natoa pole kwa familia, Clouds Media Group, ndugu, jamaa na marafiki kwa msiba huu mzito,” ameandika Majizzo.

Ukiacha utangazaji, Gardner amewahi kuwa Meneja wa mwanamuziki Lady Jaydee ambaye pia alikuwa mke wake.

Ndoa ya wawili hao ilidumu kwa takribani miaka 10 kabla ya kutalikiana.

Gardner na Lady Jaydee walifunga ndoa Mei 2005 na ilipofika Desemba 2016 ilitolewa talaka ukawa mwisho wa ndoa yao iliyovuta hisia za wengi tangu ilipofungwa kutokana na ushawishi wa wawili hao.

Hata hivyo, waliendelea kushirikiana katika mambo mbalimbali, mathalani Oktoba 2023 Lady Jaydee alihudhuria kipindi cha Jahazi na kumpatia Gardner zawadi ya viatu alivyomnunulia nchini Marekani. Novemba 2023 akampa zawadi ya manukato.

Wanamuziki kupitia mitandao ya kijamii wametoa salamu za pole kutokana na kifo cha Gardner, miongoni mwao ni Chege aliyeeleza jinsi alivyomtoa kimuziki.

“Upo katika historia ya safari yangu ya muziki, uliacha kila jambo lako la msingi ukaja studio kwa Master J chini ya Prodyuza (mtayarishaji muziki) Miikka Mwamba. Ulisimamia kuanzia utunzi mpaka tunarekodi na ukaondoka na demo ya wimbo wangu ulonitambulisha kwenye ‘gemu’ ya Bongofleva, Twenzetu,” ameandika Chege ambaye pia alitamba na kundi la TMK Wanaume. 

Ameandika: “Kupitia Clouds FM wimbo mliucheza kwa siku zaidi ya mara 10, Mungu akasimamia wimbo ukavuma sana.”

Mwigizaji Batuli ameandika:  “Jahazi limezama na hakuna neno linaloweza kubadili hili au kufuta maumivu ya kumpoteza baba na kaka yetu nguli na mahiri kwenye utangazaji.”

“Salaam zangu za pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki, pole za dhati kwa Malkia Karen na Clouds FM. Mwenyezi Mungu awape subira na uvumilivu mkubwa.”

Kwa upande wake AY ameandika: “Kutoka kuongea na wewe jana (Aprili 19) na leo kusikia umefariki, kiukweli nimeumia sana. Lala salama kaka, Mungu akulaze mahali pema peponi.”

“Eeeh Mungu, kazi yako haina makosa, pumzika salama kaka, asante kwa upendo wako. Mungu akulaze mahala pema peponi,” ameandika Mr. Blue kupitia Instagram.

Msanii wa Bongofleva, Matonya amewahi kueleza Gardner ndiye mtu wa kwanza kusikiliza wimbo wake ‘Anita’ kabla haujakamilika. Gardner aliupenda ndipo akafanya mpango Lady Jaydee akasikika katika wimbo huo uliobeba jina la albamu yake ya tatu.

Mshereheshaji Mc Garab akizungumza na Mwananchi Digital amesema amepokea taarifa za kifo cha Gardner kwa masikitiko makubwa.

“Nimeshutushwa sana na kifo cha Gardner, kwangu alikuwa inspiration kabla hatujafamiana mwaka 2021 niliwahi kum-post Facebook na mwaka 2020 nikaikuta ile kumbukumbu wakati huo  tulikuwa tumeshafahamiana na kuwa marafiki, hivyo nikamtumia ile post na akaniambia anajisikia fahari kupitia kipaji changu alikuwa ananikubali,” amesema.

Amesema Gardner aliwahi kumweleza kuhusu ugonjwa uliokuwa ukimsumbua na kumtaka amuombee katika safari ya matibabu.

“Kitu ambacho watu hawakifahamu kwamba G alikuwa anaishi maisha yake na alikuwa na furaha, wakati tulivyokuwa tunakutana sehemu za starehe nilikuwa nikimweleza simuelewi katika upande wa afya naye alikiri kuwa yupo kwenye matibabu, ila nimuombe heri tu” amesema McGarab.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso ameeleza amepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo cha kaka na rafiki yake Gardner.

“Ni habari ngumu sana kuzihimili, lakini kwa hakika hayo ndiyo mapenzi ya Mungu. Nitoe pole kwa familia yake, familia ya Clouds Media, ndugu jamaa na marafiki na wote walioguswa na msiba huu mkubwa,” ameandika Aweso.

“Tutaikumbuka daima sauti yake adhimu na adimu, umahiri wake na ufanisi katika kazi yake aliyoifanya maisha yake yote na kuacha alama itakayodumu ya utangazaji.”

“Nimeshtushwa, nimeumia na nimesikitishwa sana na kifo cha kaka Gardner G. Habash, mtangazaji mwandamizi wa vyombo vya habari vya Clouds. Lala salama, umefanya mengi katika tasnia yetu ya habari. Mwendo umeumaliza, huna baya. Poleni familia, Clouds Media, ndugu, jamaa na marafiki,” ameandika Gerson Msigwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Related Posts