KIKOSI cha Yanga jana jioni kilikuwa uwanjani kuvaana na Copco ya Mwanza katika pambano la kiporo cha michuano ya Kombe la Shirikisho, huku kocha wa timu hiyo, Sead Ramovic akiwatega mastaa wa timu hiyo akiwamo Pacome Zouzoua, Yao Kouassi na Prince Dube.
Kocha huyo raia wa Ujerumani, amewatumia mastaa hao ujumbe na wengine wa timu hiyo mapema kwa kuwataka wakae kwa kutulia kwani anaenda kusaka kikosi kipya kwa ajili ya msimu ujao, hivyo kila mechi watakaopewa nafasi kucheza, waitumie kwa akili ili panga lisije likawapitia.
Ramovic, aliyetua Yanga Novemba mwaka jana kuchukua nafasi ya Miguel Gamondi aliyefurushwa baada ya timu hiyo kupoteza mechi mbili mfululizo za Ligi Kuu mbele ya Azam FC na Tabora United, licha ya kuifikisha timu makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa msimu wa pili mfululizo.
Tangu ajiunge na Yanga, kocha huyo ameiongoza katika mechi 11, zikiwamo tano za Ligi Kuu alizoshinda zote na sita za Ligi ya Mabingwa Afrika na alishinda mbili, sare mbili na kupoteza mbili, huku timu hiyo ikishindwa kwenda robo fainali kutokana na kuvuna pointi nane tu.
Kocha huyo alisema, wakati Ligi Kuu Bara ikianza mwezi ujao sambamba na kuwepo kwa mechi za Kombe la Shirikisho, ni wakati wa yeye na jopo lake la benchi la ufundi kuanza msako wa kikosi kipya atakachoanza nacho upya msimu ujao baada ya safari hii kuikuta timu katikati ya mashindano.
Alisema kiu ya kila mwanayanga ni kutaka kuona Yanga inafanya vyema katika michuano ya ndani ili irudi kimataifa na anataka kuhakikisha anakuwa na kikosi bora kitakachohimili michuano hiyo na kazi ataianza sasa kwa mechi zote zilizosalia za michuano ya ndani baada ya kukwama kimataifa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ramovic alisema kwa sasa, anarejea katika ukali na kuwatahadharisha wachezaji wa timu hiyo, hatakuwa na mchezo na mtu kwa sababu hataki kupata aibu nyingine tena.
Alisema ameshaichungulia ratiba ya Ligi Kuu na kubaini itakuwa ngumu kwa sababu watakuwa na mechi za karibu karibu, lakini njia bora ya kukabiliana na hilo ni kila mchezaji kuwa tayari.
“Nimewaambia wachezaji wangu nitakuwa na mabadiliko ya kikosi katika mechi zote na hilo ni kwa walio tayari pekee na kama hautakuwa tayari ni sawa na kujiweka kando,” alisema Ramovic na kuongeza;
“Na hapa ndiyo naanza kupiga hesabu za kikosi changu kwa msimu ujao. Nimewaambia nataka kuwa na wachezaji washindani kupitia kundi la mastaa 25 nililonalo. Mechi hizi zitanisaidia kufanya maamuzi ya watu gani nataka kubaki nao kwa msimu ujao na wangapi wa kuwacha.”
Kocha huyo aliyeiongoza Yanga kushinda mechi tano mfululizo wa Ligi Kuu na kuvuna jumla ya mabao 18 na kufungwa mawili, alisema hataangalia ukubwa wa jina la mchezaji, kwani atakuwa mkali kwa yeyote atakayezingua kwa vile anataka kumaliza msimu vizuri na kuanza msimu mpya akiwa kivingine kabisa.
Yanga itaanza mechi za duru la pili la Ligi Kuu Bara kwa kula kiporo dhidi ya Kagera Sugar wikiendi ijayo kabla ya kucheza mechi nyingine ndani ya Februari na kusubiri kuja kuvaana na watani wao, Simba katika Dabi ya Kariakoo itakayipigwa Machi 8, likiwa pambano la kwanza kwa kocha huyo dhidi ya Mnyama.
Katika mechi ya kwanza iliyopigwa Oktoba 19, Yanga ilishinda kwa bao 1-0 la kujifunga la beki wa Simba, Kelvin Kijili, kikosi wakati huo kikiwa chini ya kocha Miguel Gamondi.