Anti nashindwa kumuelewa mume niliyenaye na hiki kinanipa shida sana. Huu ni mwaka wa sita nipo naye hajawahi kunisifua nikipendeza wala kunikosoa nisipopendeza. Ilimradi tunaishi tu. Huwa naona wivu sana wenzangu wanapotakiwa heri ya kuzaliwa au kumbukumbu ya ndoa zao, kwani kwangu hayo ni historia, haijawahi kutokea mume wangu akayazungumzia.
Nilijaribu kufanya hili na lile kuadhimisha kumbukumbu ya siku tuliyofunga ndoa naona kama namchosha, kwani haoni umuhimu.
Hayo yote hayanipi shida kuzidi anavyoishi na mimi bila kunisifia, hicho kitu kinaniuma sana. Sijui nifanyeje, nahisi kuichukia ndoa. Naomba kujua kama mtu anaweza kukupenda na asikusifie hata siku moja.
Pole sana kwa kutamani usichokipata. Ila kwanza kabisa unatakiwa kujua binadamu wanatofautiana, hususan wanaume. Wapo wanaojieleza sana wakimpenda mtu na wapo wanaopenda kimyakimya ila mapenzi ya dhati.
Kibinadamu kutosifiwa na mumeo kweli kunaweza kusababisha maswali mengi kuhusu anavyokupenda na kukuthamini. Ni kawaida kutaka kupata uthibitisho wa upendo kupitia maneno ya sifa na kuelezwa mambo mazuri na mwenza wako.
Hata hivyo, ni muhimu kuelewa kuwa upendo unajidhihirisha kwa njia nyingi tofauti, na si lazima kupitia sifa za moja kwa moja.
Jambo muhimu unaloweza kufanya kupima hilo ni kuangalia jinsi mume wako anavyowasiliana na wewe katika njia nyingine. Upendo unaweza kuonyeshwa kupitia vitendo, siyo tu maneno. Huenda anajitahidi kukutimizia mahitaji yako ya kihisia au kifedha, au pengine anajitahidi kuhakikisha kwamba unapata furaha katika mambo ya kila siku. Katika hali kama hizi, upendo wake unaweza kuwa wa kimya, lakini wenye nguvu.
Wakati mwingine, watu hawajui jinsi ya kutoa sifa au hata wanaweza kuwa na hisia zao za ndani ikawa ngumu kueleweka. Mume wako anaweza kuwa na mazingira au malezi ambayo hayakuweka msisitizo kwenye kutoa sifa au kujielezaeleza, lakini hiyo haimaanishi hakupendi.
Hujasema kama hamna mawasiliano mazuri, anakunyima hiki na kile. Malalamiko yako ni kutoambiwa unapendwa, umependeza. Binafsi nakuelewa ila kama anatimiza wajibu wake katika kila jambo ujue anakupenda ila si mtu wa kujieza.
Siku zote kumbuka na uzoee kuwa watu wana mitazamo tofauti kuhusu jinsi wanavyopaswa kuonyesha upendo. Baadhi ya watu wanapenda kutoa sifa na pongezi, wakati wengine wanaweza kujiona hawana ujuzi huo.
Ukuaji wa mtu binafsi na maendeleo ya kihisia yanaweza pia kuathiri jinsi tunavyojieleza katika uhusiano. Inawezekana kuwa mume wako anahitaji muda wa kujifunza jinsi ya kutoa sifa, au huenda anaona ni vigumu kutokana na mambo aliyoyapitia maishani.
Pia kuna mambo wanaume huwa wanazungumza kwenye vikao vyao. Mojawapo ni kuambiana kuwa mwanamke ukimpenda akijua atakusumbua. Pengine mumeo hasemi ila anajihami usije kujua anakupenda ukaanza kumringia na kumsugua nafsi, ndiyo maana anakupenda kimya kimya.
Ikumbukwe pia kwamba kadiri mtakavyozidi kuwa pamoja, kuna uwezekano kuwa mume wako atajua jinsi ya kutoa sifa kwa urahisi zaidi. Uhusiano unahitaji muda na uvumilivu. Kuna wakati ambapo mume wako anaweza kufikiria kuwa wewe tayari unajua ni kiasi gani anakupenda, hivyo anajizuia kutoa sifa akidhani kwamba sio muhimu.
Muhimu kutoa nafasi kwa mume wako kuelezea hisia zake kwa njia yake. Ni muhimu pia kujiuliza, je, wewe mwenyewe unatoa sifa kwa mume wako? Hili linaweza kuwa suala la pande zote ambapo huenda umejikita zaidi katika kutaka sifa kutoka kwake, na huenda hukutambua kwamba ni muhimu pia wewe kumhimiza na kumuonyesha sifa.
Uhusiano mzuri unajengwa kwenye ushirikiano na kuelewana, hivyo kutoa na kupokea sifa husaidia kuimarisha mahusiano yenu. Hivyo anza kumsifia yeye, kumshukuru na kumueleza hisia zako kadiri unavyoweza.
Baada ya muda ukiona amezoea hali hiyo mwambie waziwazi kuwa unapenda kuelezwa kama umependeza au umepuyanga.
Siku nyingine ukivaa muulize kama umependeza, hakikisha anajibu hilo swali, huku unazungukazunguka. Nenda naye taratibu, mwisho atazoea.
Usikae ukasubiri aote, muulize, mwambie unaamini kusikia sifa kutoka kwake, mwambie lolote unalotamani kutoka kwake lililo ndani ya uwezo wake. Ndiyo mumeo huyu, tamba naye kwa kusemezana usikae kimya