Mmiliki Alliance afariki dunia, kuzikwa Februari 2

MMILIKI wa timu za Alliance FC na Alliance Girls za Mwanza, James Bwire amefariki dunia usiku wa kuamkia leo Jumapili (Januari 26, 2025) wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando.

Bwire ambaye ni mdau mkubwa wa michezo nchini akiwa ni Mkurugenzi wa Kituo cha Kukuza na Kulea vipaji cha Alliance aliwahi pia kuwa mwanasiasa akiwa Diwani wa Kata ya Mahina Jimbo la Nyamagana na Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Mashindano kituo cha Alliance, Stephano Nyaitati,  ni kwamba Bwire amefikwa na umati baada ya kushambuliwa na kiharusi saa 3 usiku jana Jumamosi akiwa nyumbani kwake na kukimbizwa Hospitali ya Bugando ambapo alifariki saa 4 usiku baada ya kupokelewa kitengo cha dharura.

Amesema Bwire alikuwa na changamoto ya kuumwa kwa muda mrefu kutokana na matatizo ya presha ambapo hivi karibuni alipelekwa India kupata matibabu na afya yake kuimarika, lakini jana hali ilibadilika ghafla na kusababisha kifo chake.

“Ni kweli mkurugenzi wetu ambaye ndiyo muasisi wa Shule na Kituo cha Michezo cha Alliance amefariki dunia. Alikuwa ni mgonjwa kwa muda kidogo alipata changamoto kidogo utakumbuka kuna mwaka hapo nyuma alishakwenda India akapata matibabu alikuwa anaendelea vizuri,” amesema Nyaitati na kuongeza;

“Alikuwa na changamoto ya presha lakini hali yake ilibadilika jana (jumamosi) majira ya saa tatu usiku akiwa nyumbani kwake baada ya kushikwa na Kiharusi, tukafanya utaratibu wa kumpeleka hospitalini, baada ya kufika hospitali ya Bugando ikabainika ameshafariki.”

Nyaitati alisema uongozi wa kituo cha Alliance umekubaliana kufanya mazishi ya mwasisi wao huyo Jumapili Februari 2, mwaka huu, huku akiwakaribisha ndugu, jamaa na marafiki kushirikiana kuhakikisha mpendwa wao huyo anastiriwa vizuri.

“Kama unavyojua mzee Bwire ni mtu wa watu amefanya kazi Serikalini na kulitumikia Jiji la Mwanza amekitumikia pia chama (CCM) na kwenye mpira amefanya mambo makubwa, kwahiyo sisi kama familia ya Alliance tumekubaliana kwamba maziko yake tutayafanya siku ya Jumapili wiki ijayo (Februari 2),” amesema Nyaitati na kuongeza;

“Kwa sasahivi kwa watu ambao ni ndugu, jamaa na marafiki wafike nyumbani kwa ajili ya kuomboleza na kuendelea kushirikiana kwa pamoja kuhakikisha kwamba tunamsitiri vizuri.”

Alliance FC ilianzishwa mwaka 2012 na kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa mwaka 2018/2019 na baadaye kushuka daraja ambapo kwa sasa inashiriki First League. Timu hiyo imetoa wachezaji mbalimbali akiwemo Israel Mwenda, Zabona Mayombya, Juma Nyangi, Hans Masoud na Balama Mapinduzi (Kipenseli).

Alliance Girls ilianzishwa mwaka 2016 na inashiriki Ligi Kuu ya Wanawake tangu mwaka 2017  na hadi sasa ikiwa imewaibua nyota mbalimbali wanaotamba ndani na nje ya nchi wakiwemo, Aisha Masaka (Brighton &Holves Albion), Aisha Mnunka (Simba Queens), Enekia Kasonga (Uturuki), Winfrida Charles (Fountain Gate) na Aliya Fikiri (JKT Queens).

Related Posts