Nafasi ya nishati ya uhakika kwa maendeleo ya Afrika

Dar es Salaam. Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Amina Mohammed, ametaja maeneo manne yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa kikamilifu.

Maeneo hayo ni pamoja na kutengeneza mazingira mazuri ya sera yanayowiana, mifumo, fedha, na taasisi imara.

Amesema hayo leo Jumatatu, Januari 27, 2025, wakati akitoa hotuba katika mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika kuhusu nishati unaolenga kutoka na maazimio yatakayowezesha Waafrika milioni 300 kufikishiwa huduma ya umeme ifikapo mwaka 2030.

Amina amesema ni vema kuwapo kwa mazingira ya kisera yanayowiana huku akieleza kuwa wakati mwingine nchi inaweza kuwa na mazingira sahihi ya sera, lakini vyombo vya usimamizi vinaleta changamoto.

“Taasisi zinafanya nini na watungaji wa sheria? Unaweza kukuta mchakato unakuwa mkubwa, kinachoturudisha nyuma ni muda mrefu unaotumika kuhakikisha tuna sheria sahihi na Serikali kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji kuja. Tunapojaribu kuzisaidia nchi kuweza kuungana lazima zitengeneze mazingira ya kisera,” amesema.

Pia amesema mazungumzo katika mkutano huo yasijikite tu kwenye nishati bali pia kwenye vitu vitakavyounganishwa ndani yake, hivyo ni muhimu kuwapo kwa mifumo ya chakula itakayowezeshwa na nishati inayotengenezwa.

“Tunapozungumzia uzalishaji wa chakula, ni maeneo ya vijijini ndipo tutakapokutana na wanawake na vijana watakaofurahia umeme uliounganishwa. Pia teknolojia, huduma za kifedha kwa wanawake, ugavi, na biashara kukua, lazima teknolojia iwepo ili kuungana na mifumo ya chakula.

“Hii itasaidia kuimarisha ulinzi wa kijamii na kuwepo kwa sheria zinazozuia changamoto za mabadiliko ya tabianchi,” amesema.

Kuhusu fedha, amesema kuna pande mbili: rasilimali za ndani ya nchi na fedha zinazoweza kupatikana kutoka vyanzo mbalimbali. Ni lazima sekta binafsi ipewe nafasi kwa kuweka mazingira wezeshi.

“Ni vyema kuangalia mazingira ya kugharamia fedha yakoje. Nchi za G20 zinafanya nini ili kuleta uwekezaji mkubwa? Kuleta mifumo ya kugharamia nishati si jambo jepesi kwani kunahitaji watu wengi, wabia, wasimamizi wa sheria na sera. Vyote hivi lazima viwe pamoja,” amesema Amina.

Kwa upande wa taasisi, amesema si tu kuwajengea watu binafsi uwezo, bali pia kuhakikisha mifumo ya kiserikali, utawala, wizara, na sekta mbalimbali zinafanya kazi kwa pamoja.

“Hatuwezi kusubiri kuzijenga na kusema zitajitegemea zenyewe. Lazima ziwe endelevu, lakini wengi hawapendi kuweka fedha katika kutengeneza taasisi,” amesema.

Amesema kuwajengea watu uwezo ni rahisi, lakini kujenga taasisi ni changamoto kubwa. Hata hivyo, kuna njia nyingi bunifu za kuhakikisha taasisi zinaimarika.

“Lazima kuwe na mipango. Kama si mpango wa maendeleo, basi mpango wa nishati. Jamii ya kimataifa inazipa nchi mipango mingi isiyo na mwisho. Kwa nini tusizipe nguvu taasisi zikaweza kufanya hivyo? Kwa mfano, hapa Tanzania,” amesema.

Kuhusu mkutano huo, Amina amesema Ajenda 300 inaonyesha uongozi thabiti kutoka mashirika ya fedha makubwa duniani. Ameongeza kuwa changamoto zipo, lakini jitihada zaidi zinahitajika kufanikisha malengo.

Amesema ni lazima kuwepo na mfumo endelevu wa kugharamia miradi mikubwa, huku nchi za Afrika zikishirikiana kuangalia fursa zinazopatikana, ikiwemo ajira kwa vijana, wanawake, na kukuza utu wa mtu.

“Tuna migogoro mingi inayoendelea katika Bara hili. Kama hatuwezi kuleta nishati katika maisha ya watu ili wafanye shughuli zao, basi ni vigumu kuona amani na kuweka bunduki pembeni,” amesema Amina.

Amesisitiza kuwa, ili uchumi uwe stahimilivu ifikapo 2030, ni lazima kuwepo na nishati ya uhakika.

Related Posts