Unguja. Kaimu Kamishna Mkuu Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA), Saidi Ali Mohammed amesema bado nchi za Afrika zinakabiliwa na changamoto za risiti za kielektroniki kwani wafanyabiashara hawana mwamko wa kutoa risiti na wananchi hawazidai pia.
Amesema hiyo ndio sababu ya mapato ya Serikali kutokusanywa vizuri, hivyo uwepo wa mkutano wa wadau wa kodi utaelezea mbinu mbalimbali ambazo wamechukua katika nchi zao kuhakikisha wanatokomeza changamoto hiyo.
Kauli hiyo ameitoa leo Januari 27, 2025 wakati akizungumza katika mkutano wa 98 wa wadau wa kodi wa nchi za Afrika Mashariki uliofanyika kisiwani Zanzibar.
“Risiti za kielektroniki bado kwa wananchi na wafanyabiashara wanaona ni tatizo kwa kutokuwa na mwamko wa kudai na kutoa, hivyo tuna mpango wa kutoa elimu kwa lengo la kuondokana na tatizo hilo,” amesema Said.
Amesisitiza lengo la mkutano huo ni kukaa pamoja na wadau wa nchi za Afrika kutatua changamoto zinazofanana kwa kubadilishana uzoefu na waliofanikiwa ili na wengine watumie njia zao.
Pia, amesema wamekaa pamoja kujadili njia mbadala za kuondoa biashara za magendo nchini, kwani bado zinaendelea kufanyika.
Hata hivyo, amesema kufikiwa kwa lengo la ukusanyaji wa mapato katika mamlaka hiyo isiwe sababu ya ukwepaji kodi kwa wengine, kwani Serikali bado ina mahitaji makubwa katika kodi.
Sambamba na hilo, ametoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara kutoa na kudai risiti za kielektroniki ili kukusanya kodi kwa ufanisi.
Naye, Mwenyekiti wa kamati za ufundi wa nchi za wanachama wa Jumuiya za Afrika Mashariki, Beatus Nchota amesema katika jumuiya hiyo kuna ukwepaji kodi hususan katika bidhaa za forodha za ndani, hivyo mkutano huo utabainisha bidhaa ambazo zinakwepa kodi zaidi kwa kuelezea sababu zao.
Amesema, endapo watajua sababu za ukwepaji kodi katika bidhaa hizo zitawasaidia kutengeneza mikakati juu ya bidhaa kwa lengo la kulipiwa kodi.
“Tayari tuna sheria moja za forodha katika nchi hizi ili kuzuia ukwepaji wa kodi na imetoa viwango vya kutoza, changamoto inatokea kwa nchi mojawapo kuwa na viwango tofauti na nchi nyingine bado hawajaanza kutoza viwango hivyo,” amesema Nchota.
Akitolea mfano Kenya ni nchi mojawapo iliyoanza kutoza kodi katika bidhaa zinazotengenezwa pombe kali, ilhali nchi nyingine hazijaanza hivyo changamoto inatokea hapo.
Amesema kupitia mkutano huo watajadili na kuweka viwango sawa ili kukwepa mianya hiyo ya ulipaji kodi na ipo kamati maalumu ya kutengeneza sheria ya kulipa kwa pamoja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Utafiti na Mipango kutoka ZRA, Ahmed Haji Saadat amesema kupitia mkutano huo watajifunza uzoefu kwa wenzao na kupata jawabu ya changamoto zinazowakabili.
“Kila nchi itawasilisha ukusanyaji wa mapato kwa kipindi cha miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba, kwa kuangalia changamoto na njia walizotumia kuzitatua.
Vilevile amesema kwa sasa mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto ya uwajibikaji mdogo wa usajili kwa wafanyabiashara.
Pia, amesema baadhi ya wafanyabiashara ambao wamesajiliwa wanakwepa kulipa kodi licha ya kusajiliwa kwao.