Waasi wa M23 wanaelezwa kuungwa mkono na Rwanda wametangaza kuwa wameukamata mji mkubwa wa Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), mapema leo Jumatatu.
Taarifa hiyo ilitolewa dakika chache kabla ya muda wa saa 48 zilizotolewa na jeshi la Kongo kusalimisha silaha kumalizika.
Waasi hao wamewahimiza raia wa Goma kuwa watulivu huku wakitoa wito kwa wanajeshi wa Kongo kujisalimisha kwenye uwanja wa michezo wa mji huo.
Taarifa za Human Rights Watch zinaonya kuwa mzozo huu unaweza kusababisha janga kubwa la kibinadamu. Walinda amani wa Umoja wa Mataifa walianza kuwasajili askari waliojisalimisha viungani mwa Goma Jumapili usiku.
Msemaji wa serikali ya Kongo, Patrick Muyaya, amesema kuwa hali ya usalama inabadilika mara kwa mara na ameomba juhudi za ziada zifanyike.
Wakazi walisambaza video za waasi wa M23 wakishika doria katika mitaa mikuu ya Goma kufuatia msururu wa mashambulizi dhidi ya jeshi la Congo siku ya Jumapili na kuwashuhudia makumi ya maelfu ya watu wakikimbilia miji jirani.
Hata hivyo kwa upande wake serikali ya Congo inasisitiza kuwa bado inadhibiti sehemu za kimkakati za mji huo. Imeishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa kutuma wanajeshi kuvuka mpaka kusaidia M23. Kigali inakanusha hilo.
Rwanda inasema Kinshasa inaunga mkono wanamgambo wanaotaka mabadiliko ya utawala mjini Kigali.
Lakini katika mkutano wa Umoja wa Mataifa Uingereza Marekani na Ufaransa ziliilaani Rwanda kwa kuunga mkono hatua hiyo, na baraza la usalama lilitaka kuondolewa kwa vikosi vya nje nchini Congo.