Dk Rugazia: Eneo la jinai linawasumbua wananchi

Na Mwandishi Wetu

WAKILI wa Kujitegemea Dk Aloys Rugazia amesema eneo la jinai la kubambikiwa kesi ni eneo ambalo linasumbua watu wengi katika jamii, wananchi wamekuwa wakilalamika kwamba hiyo ni changamoto wanayokutana nayo katika maisha yao.

Dk Rugazia amesema hayo leo katika viwanja vya Shule ya Sekondari Kibasila iliyopo jijini Dar es Salaam wakati wa maandalizi ya kutoa elimu ya sheria bure na kuandaa nyaraka katika kuadhimisha wiki ya sheria kwa lengo la kuwafikia wananchi ambao hawana fedha za kupata huduma za sheria.

“Tunapokutana na wananchi wanatueleza changamoto nyingi katika eneo la jinai kwamba kuna kubambikiwa kesi kuna kuonewa ndiyo maana tunawataka waje hapa tuwape elimu ya kutosha wajue haki zao ni zipi na watakiwa kufanya nini,” amesema Dk Rugazia

Aidha, amesema changamoto nyingine ambayo wananchi wanapata ni eneo la ardhi na mirathi wajane, wazee na watoto yatima wanapata shida kupata haki zao za msingi kwa wakati.

“Ardhi ni maisha ni moja kati ya mali muhimu katika mustakabali wa watu mara nyingi ardhi imekuwa ikileta msuguano waliyonacho na wasio nacho, mara nyingi wanajikuta katika hali ngumu ndiyo maana kwa wiki hii tunatoa msaada bure watu waje,” amesema Dk Rugazia

Amesema kuwa wapo kwenye wiki ya sheria ambayo ilizinduliwa Januari 25, 2025 kwa kawaida wanaadhimisha kwa kujaribu kuifikia jamii kuhakikisha inapata haki kwa sababu sio kila mtu anauwezo wa kulipia gharama za kupata huduma za kisheria.

“Hivi karibuni Rais alianzisha Mama Samia Legal Aid mpango mkakati wa kuweza kutoa msaada wa kisheria kwa watu ambao tunaishi nao katika jamii yetu na kwa namna moja au nyingine wana kiu ya haki lakini hawawezi kuipata,”.

Wakili wa Kujitegemea Dk Aloys Rugazia akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) katika Viwanja vya Shule ya Sekondari Kibasila iliyopo Temeke jijini Dar es Salaam wakati wa maandalizi ya Kampuni ya Sheria Afrifa Legal Consultant ya kutoa elimu kwa wananchi bure.
 

Related Posts