Dar es Salaam. Ngwe ya kwanza ya mkutano wa wakuu wa nchi Afrika kuhusu nishati imekamilika na kuibua matumaini ya kufikiwa kwa lengo tarajiwa, huku Serikali za Afrika zikitwishwa mzigo wa masuala ya kisera zinayopaswa kuyafanyia kazi.
Matumaini ya kufikiwa kwa malengo hayo yanatokana na ahadi za fedha kutoka taasisi mbalimbali za kifedha, kuwezesha utekelezaji wa ajenda ya kufikisha umeme kwa watu milioni 300 katika mataifa ya Afrika ifikapo 2030.
Hata hivyo, jukumu lililoko mbele ya Serikali za Afrika ni kuhakikisha zinaboresha mazingira ya kisera na kisheria, kuhakikisha uwekezaji katika sekta ya nishati hasa mbadala unawezekana.
Mkutano huo unaowakutanisha wakuu wa nchi 25 wa Afrika na wakuu wa taasisi mbalimbali duniani unalenga kukomesha giza katika bara hilo na kuhakikisha usambazaji wa nishati unawezekana.
Katika hatua za awali za utekelezaji wa Ajenda 300, mataifa 14 ya Afrika yatasaini mkataba wa kuridhia hilo, ratiba ambayo inatarajiwa kutekelezwa katika ngwe ya pili itakayotamatisha mkutano huo, kesho Januari 28, 2025.
Akizungumzia vikwazo vya uwekezaji katika nishati mbadala Afrika, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Nishati Mbadala (IRENA), Francesco La Camera, amesema kuna uhaba wa miundombinu.
Amesema kukosekana kwa miundombinu kunamfanya mwekezaji kukosa uhakika wa uzalishaji au wakati mwingine atumie gharama kubwa kuwekeza.
Eneo hilo ni miongoni mwa yale aliyoyataja kuwa taasisi za fedha zinapaswa kuwekeza juhudi zao kuisaidia Afrika, ili kutengeneza mazingira yatakayoshawishi mtaji wa sekta binafsi.
Kukosekana kwa soko la nishati mbadala ni kikwazo kingine kilichotajwa na La Camera katika uwekezaji wa nishati hiyo barani Afrika.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, soko la Afrika limetengenezwa kujikita katika aina moja ya nishati, hivyo inawapa ugumu wawekezaji wa nishati mbadala kufikiria kuwekeza.
“Mnapaswa kufanyia kazi mazingira ya kisera na sheria yatakayofungua soko la nishati mbadala Afrika, hapo wawekezaji watavutiwa na kuja kwa wingi,” amesema.
Sambamba na hayo, ametaja sababu nyingine ni kukosekana kwa taasisi na wataalamu wenye uwezo wa kusimamia nishati mbadala.
“Kunapaswa kuwa na taasisi na wataalamu wanaoweza kusimamia masuala ya nishati mbadala, badala ya zile zinazojua kuhusu nishati ya mafuta pekee,” amesema.