Unguja. Wakati Mkutano wa 15 wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar ukianza kesho, shughuli zinazotarajiwa kufanyika ni majadiliano ya bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25.
Mbali na bajeti, miswada miwili ya sheria itawasilishwa na kujadiliwa, mwingine ukiwa uliosomwa kwa mara ya kwanza katika mkutano wa 14.
Miswada hiyo ni wa Sheria ya Fedha, wa Sheria ya Kuidhinisha Matumzi ya Serikali kwa mwaka 2024/25 na wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria.
Mkutano huo pia utafanya marekebisho ya Kanuni za Kudumu za Baraza la Wawakilishi la Zanzibar toleo la 2020.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumanne Mei 14, 2024 wakati akitoa taarifa kuhusu mkutano huo barazani hapo, Mkurugenzi wa Shughuli za Baraza la Wawakilishi, Othman Ali Haji amesema katika mkutano huo, pia yataulizwa maswali 291 na kupatiwa majibu.
“Kama tunavyojua huu ni mkutano wa bajeti ambao Bajeti Kuu ya Serikali itawasilishwa na bajeti za wizara zote kwa hiyo mkutano huu ni muhimu kwa maendeleo ya Taifa,” amesema.
Baadhi ya wananchi waliozungumza na Mwananchi Digital wamesema wanatarajia liwe baraza ambalo wawakilishi watajielekeza kuzungumzia changamoto za wananchi badala ya masilahi binafsi.
Sheikha Ali Issa amesema, “huu ndiyo mkutano ambao umeshikilia masilahi ya wananchi na Taifa, tunategemea wawakilishi wasimame kwa wananchi na kuibana Serikali itoe maelezo kwa mambo yanayohitaji majibu kwa wananchi.
Mkazi wa Kiwengwa, Thuleiya Ahmada amesema anatamani kuona bajeti itakayokuwa inatosheleza kutatua matatizo ya wananchi, kwa kuwa iliyopita walishuhudia upungufu wa bajeti za kisekta jambo linalosababisha ufanisi mdogo.
Mwinyi Othman Said, amesema matarajio yake ni kuona Serikali inabuni vyanzo vipya vya mapato badala ya kuendelea kutegemea vilevile vya siku zote.