TIMU ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars imepangwa Kundi C katika michuano ya Afcon 2025 itakayofanyika nchini Morocco ikishirikisha timu 24.
Katika droo hiyo iliyochezeshwa leo Jumatatu Januari 27, 2025 nchini Morocco, Taifa Stars imepangwa na timu za Nigeria, Tunisia na Uganda.
Hii itakuwa mara ya nne kwa Stars kushiriki Afcon baada ya kufanya hivyo mwaka 1980 (Nigeria), 2019 (Misri) na 2023 (Ivory Coast) ambapo nyakati zote hizo imeishia makundi.
Kwa mwaka huu Stars kupangwa na Nigeria, inakumbushia Afcon 1980 iliyofanyika nchini Nigeria ambapo timu hizo zilikuwa Kundi A ambapo zilipokutana katika mchezo wa kwanza Nigeria ilishinda 3-1. Kipindi hicho michuano hiyo ilishirikisha timu nane pekee.
Michuano hiyo ambayo mwaka huu itakuwa ni msimu wa 35, imepangwa kufanyika nchini Morocco kuanzia Desemba 21, 2025 mpaka Januari 18, 2026 ambapo fainali itafanyika Dimba la Prince Moulay Abdellah.
Wakati Stars ikiwa Kundi C, mabingwa watetezi Ivory Coast wamepangwa Kundi F na timu za Cameroon, Gabon na Msumbiji huku wenyeji Morocco wapo Kundi A na Mali, Zambia na Comoros.
Makundi yote sita yapo hivi;
Kundi A: Morocco, Mali, Zambia, Comoros
Kundi B: Misri, Afrika Kusini, Angola, Zimbabwe
Kundi C: Nigeria, Tunisia, Uganda, Tanzania
Kundi D: Senegal, DR Congo, Benin, Botswana
Kundi E: Algeria, Burkina Faso, Equatorial Guinea, Sudan
Kundi F: Ivory Coast, Cameroon, Gabon, Msumbiji