KUNA wachezaji watatu ndani ya kikosi cha Yanga walioibua presha mpya inayoweza kubadilisha upepo ndani ya timu hiyo siku chache zijazo wakati Ligi Kuu Bara itakaporejea.
Wachezaji hao watatu ni winga mpya, Jonathan Ikangalombo ‘Ikanga Speed’, beki wa Israel Mwenda na kiungo mshambuliaji Maxi Mpia Nzengeli, ambao wameibua presha kwa nyota waliokuwa wakitumika katika nafasi wanazocheza mashine hizo, japo jukumu zima lipo mikononi mwa Kocha Sead Ramovic.
Tuanze na Mwenda, beki huyo wa pembeni aliyesajiliwa na Yanga dirisha dogo la usajili akitokea Singida Black Stars, ana uwezo mkubwa wa kucheza nafasi zote mbili za beki wa pembeni kwa maana ya beki wa kulia na beki wa kushoto na kiwango alichokionyesha katika mchezo wa kwanza akiwa na kikosi hicho wakati wakiigonga Copco kwa mabao 5-0 mechi ya Kombe la Shirikisho ni kama katuma salamu tosha.
Kama Ramovic ataamua kumtumia Mwenda upande wa beki wa kulia, maana yake mmojawapo kati yake, Kibwana Shomari na Yao Kouassi atajikuta katika wakati mgumu wa kupata nafasi katika kikosi cha kwanza cha Yanga.
Uhalisia ni hakuna uwezekano wa kocha kuwatumia wachezaji watatu wa nafasi ya beki wa kulia kwa wakati mmoja maana yake utasababisha mmoja kukaa jukwaani na wengine wawili kutumika katika mchezo mmoja kwa mmoja kucheza na mwingine kuwepo benchi.
Kungekuwa na uwezekano wa Mwenda au Yao mmojawapo kutumika katika nafasi ya winga wa kulia lakini uwepo wa idadi kubwa ya wachezaji wanaomudu kucheza katika nafasi hiyo, unazidi kuweka kikwazo kwa hilo kutokea.
Ni kama itakavyokuwa katika upande wa beki wa kushoto ambako pia Mwenda anamudu kucheza kwani kuna Nickson Kibabage na Chadrack Boka ambao kabla hata ya dirisha dogo la usajili walikuwa wanagawana dakika za kucheza ndani ya timu hiyo.
Kwa usajili wa winga, Ikanga Speed unaweza kuibadilisha Yanga katika namna mbili ambazo ni upangaji wa kikosi na mfumo wa kiuchezaji iwapo mchezaji huyo atafanikiwa kulishawishi benchi la ufundi la timu hiyo. Licha ya kuwa, bado hajaanza kuitumikia timu hiyo baada ya kuugua ghafla kabla ya mechi ya kiporo ya Kombe la Shirikisho, ila mashabiki wa Yanga wameweka imani kubwa kwa rekodi alizotoka nazo AS Vita ya DR Congo.
Ikanga Speed anaweza kupata nafasi ya kucheza kwa kupishana na ama Maxi Nzengeli au Stephane Aziz Ki, lakini anaweza kuifanya Yanga icheze katika mfumo wa 4-4-2 ili kumpa uhuru zaidi mchezaji huyo ambaye sifa yake kubwa ni kucheza kwa spidi. Ikanga anamudu pia kucheza kama mshambuliaji wa kati.
Kupona kwa Maxi anayetajwa kuwa mchezaji mwenye ufanisi zaidi mazoezini, kunaweza kugeuka shubiri kwa mmojawapo kati ya Clement Mzize au Prince Dube.
Kipindi Maxi alipokuwa akikosekana, kocha Ramovic alikuwa akimtumia Mzize kama kiungo mshambuliaji wa pembeni katika mfumo wa 4-2-3-1 huku Dube akisimama kama mshambuliaji wa kati.
Urejeo wa Maxi na akiwa katika ubora wake uliozoeleka maana yake utalazimisha Mzize arudishwe katika nafasi ya mshambuliaji wa kati na kwa vile mfumo wa 4-2-3-1 unahitaji mshambuliaji mmoja wa kati, hapana shaka yeye au Dube mmoja hatojikuta akianza kikosini.
Kiungo wa zamani wa Yanga, Hussein Swedi alisema anafurahia kuona wachezaji wa timu hiyo wanavyotengenezewa ushindani.
“Timu haitakiwi kuwa na wachezaji wachache ambao wanaamini watacheza kila siku kwa sababu ya kukosa ushindani. Kukiwa na vita ya kugombea nafasi ndio timu inafanikiwa kwa sababu kila mchezaji atacheza kwa kujituma na kuonyesha kiwango bora ili kumshawishi kocha kumpa nafasi,” alisema Swedi na kuongeza;
“Ukiangalia hao wachezaji uliowataja, wanaweza kucheza katika nafasi tofauti uwanjani na sio wao tu bali wapo wengi kwenye kikosi cha Yanga ambao ni viraka na wana viwango vizuri.”