Dar es Salaam. Marais wa nchi 19 na wakuu wa Serikali kadhaa tayari wamewasili nchini, kwa ajili ya mkutano wa nishati barani Afrika unaohitimisha leo jijini hapa.
Nchi ambazo marais wake tayari wamewasili Dar es Salaam kwa ajili ya mkutano huo ni Madagascar, Lesotho, Visiwa vya Comoro, Guinea Bissau, Botswana, Malawi, Burundi, Mauritania, Ghana, Ethiopia, Jamhuri ya Congo – Brazzaville, Somalia, Zambia na Gabon.
Kwa upande wa nchi zitakazowakilishwa na makamu wa Rais katika mkutano huo ni Gambia na Benin, huku Mwenyekiti wa Baraza la Rais wa Libya, Waziri wa Umeme na Nishati wa Afrika Kusini na Naibu Waziri Mkuu wa Eswatini, Waziri Mkuu wa Niger, Naibu Waziri Mkuu wa Equatorial Guinea na Djibout wakiwa miongoni mwa washiriki.
Katika mkutano wa leo, wakuu hao wa nchi wataazimia kile kilichojadiliwa katika mkutano wa mawaziri wa kisekta uliofanyika jana na nchi 14 zitasaini mkataba wa kutekeleza Ajenda300.
Kadhalika mkutano huo umewakutanisha viongozi wakuu wa mataifa mbalimbali ya Afrika na taasisi za fedha duniani.
Isingewezekana uendeshe kwa umbali wa kilomita tano au 10 kwenda katikati ya jiji, bila kukutana na askari wa usalama barabarani, sio kukagua leseni, bali kuhakikisha usalama wako.
Kasi ya mwendo wako ndio ingeamua muda wa kufika uendako, kama umechelewa si kwa sababu ya msongamano, zilikuwa shida zako.
Ile Posta ya vijiwe vya kahawa, mchana maduka usiku migahawa, ilitokomea kusikojulikana, kimya kilitawala katikati ya jiji.
Usafi ndio usiseme, hii ndio Tanzania bwana.
Ukiachana na wasimamizi wa itifaki za ulinzi, bashasha na tabasamu juu ya nyuso za wasaidizi wa mapokezi zinazoakisi ukarimu wa Watanzania na pengine kama una msongo wowote wa mawazo, unaweza kupona.
Kwa asiyependa muziki wa Kizungu, ulikuwepo wa Kiafrika, kama sio vitu vyako, kulikuwa na ngoma za asili na zikikushinda hizo, basi utaruka kimaasai.
Ilikuwa vigumu kutathmini uchumi wa mtu kwa kuangalia mavazi yake, zilivaliwa suti na mashati yaliyokolea mistari ya pasi, kila unayemwona amezingatia utanashati.
Usingekumbuka kwa haraka kama uko ndani ya Tanzania, kwani ndani lugha zilikuwa zikigongana tu. Kila utakayejaribu kuzungumza naye, angekujibu mithili ya rafiki mliyefahamiana miongo kadhaa iliyopita.
Hakukuwa na sababu ya kulalamika kwa wanahabari kutekeleza majukumu yao, kuliandaliwa chumba maalumu chenye vifaa vya kazi na kiyoyozi cha kutosha kukabili joto la Dar es salaam.
Lugha za mataifa yaliyoitawala Afrika kwa ukubwa wake, Kifaransa, Kiingereza na Kiitaliano ndizo zilizosikika zaidi, lugha pekee ya Kiafrika inayosikika ni Kiswahili.
Ule utaratibu wa muda wote ni wa chai, uliakisi uhalisia wa ukumbini, chai za vionjo tofauti zilipatikana muda wote.
Miongoni mwa jambo linalosubiriwa na wengi ni tamati ya siku ya leo kwa kuwa, kutatolewa Azimio la Dar es Salaam na nchi 14 zinatarajia kusaini mkataba wa utekelezaji wa Ajenda300.