Wakili Peter Madeleka ameshinda rufaa yake namba 263 ya mwaka 2022 aliyoikata dhidi ya Jamhuri katika Mahakama ya rufani nchini akiomba mahakama hiyo kuruhusu kupitia mienendo ya mashauri yenye shaka katika mahakama za chini. Anaripoti Regina Mkonde… (endelea).
Hatua hiyo imekuja baada ya Mahakama ya Rufaa Tanzania kutoa uamuzi uliosema kesi zinazoendelea katika mahakama za chini zenye viashiria vya kubambikiza, mienendo yake inaweza kufanyiwa marejeo na Mahakama Kuu, ili zifutwe kabla ya kumalizika, endapo ikibainika sio halali au zimefunguliwa kinyume cha sheria.
Uamuzi huo umetolewa leo Jumanne na Msajili wa Mahakama ya Rufani, katika rufaa ya jinai namba 263/2022, iliyofunguliwa mahakamani hapo na Wakili Peter Madeleka, dhidi ya Jamhuri na kusikilizwa na jopo la majaji watatu, Jaji Shaban Lila, Jaji Lugano Mwandambo na Jaji Lucia Kairo.
Katika uamuzi huo wa mahakama ya rufani, ulisema kifungu cha 372(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20, kinaipa mamlaka Mahakama Kuu kufanya marejeo wakati wowote ya kesi zinazolalamikiwa kuwa sio halali, ili zifanye maamuzi ya kuzifuta endapo zikibainika kufunguliwa kinyume cha sheria au ziendelee kusikilizwa kama itabainika ni halali.
Kifungu hicho cha 372 kinasema “Mahakama Kuu inaweza kuitisha na kuchunguza kumbukumbu ya mwenendo wowote wa kesi ya jinai iliyoko mahakama ya chini, kwa madhumuni ya kujiridhisha yenyewe kwenye usahihi, uhalali au uhakika wa matokeo, adhabu au amri iliyoandikwa au iliyopitishwa na kwenye usahihi wa mwenendo wowote wa mahakama yoyote nchini.”
Wakili Madeleka alifungua rufaa hiyo kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu, Masjala Kuu ya Dar es Salaam, katika maombi madogo ya jinai namba 359/2022, uliosema haiwezi kufanya marejeo kwenye mienendo ya kesi zinazoendeshwa na mahakama za chini, kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.
Maombi hayo madogo ya jinai yalifunguliwa na Wakili Madeleka ili kuiomba Mahakama Kuu, kufanya marejeo dhidi ya ya kutoa taarifa za uongo namba 49/2022, aliyofunguliwa na Jamhuri kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akidai si halali kwani imefunguliwa kinyume cha sheria.
Wakili huyo aliiomba Mahakama Kuu isikilize maombi yake kisha ifanye marejeo dhidi ya kesi hiyo iliyokuwa inasikilizwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Rhoda Ngimilanga na ikibainika kuwa si halali, ifutiliwe mbali.
Akizungumza na MwanaHALISI kuhusu uamuzi huo, Wakili Madeleka alisema maombi yake madogo ya kupinga kesi ya jinai aliyofunguliwa Mahakama ya Kisutu, yanarudishwa katika Mahakama Kuu kwa ajili ya kusikilizwa ili yatolewe maamuzi.
“Kwa mujibu wa uamuzi huo kesi inarudishwa mahakama kuu ili isikilize malalamiko yangu ya kupinga kesi ya jinai ya kutoa taarifa za uongo mtandaoni ambapo ninaomba mahakama hiyo iifute kwani iliingizwa mahakamani bila kufuata sheria kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo kutosajiliwa kielektroniki kwa mujibu wa sheria,” alisema Wakili Madeleka.
Wakili Madeleka aliwataka wananchi na mawakili kuutumia uamuzi huo wa mahakama ya rufani, kupinga kesi wanazoona kuwa za kubambikizwa ili zifutwe mapema kabla hazijaleta madhara kwa washtakiwa, hususan wanaoshtakiwa kwa kesi zisizokuwa na dhamana ikiwemo za utakatishaji fedha na uhujumu uchumi.
Wakili Madeleka alisema uamuzi huo unaashiria juhudi za Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, kuboresha mifumo ya haki jinai ikiwemo kukomesha kesi za kubambikiza, zinaanza kuzaa matunda.
“Mkiona uonevu wowote mkate rufaa mahakama kuu na watumie sheria hii mpya iliyowekwa na mahakama waweze kupata haki zao. Tunaamini sasa haki jinai imeanza kupata dawa taratibu taratibu,” alisema Wakili Madeleka.