NA WILLIUM PAUL, SAME.
VIONGOZI wa serikali za mitaa katika wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro wameonywa dhidi ya kuhusika katika migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji.
Onyo hili limetolewa ili kuhakikisha kuwa viongozi hao wanatekeleza majukumu yao kwa haki na kusaidia kutafuta suluhisho la kudumu badala ya kuwa chanzo cha migogoro hiyo.
Mkuu wa Wilaya hiyo, Kasilda Mgeni alitoa onyo hilo jana alipokuwa akizungumza na wananchi wa kijiji cha Marwa akiwa kwenye ziara yake katika kijiji hicho huku akisisitiza zaidi umuhimu wa viongozi wa vijiji na vitongoji kusikiliza na kutatua changamoto za wananchi kwa haki na uwazi.
“Viongozi wa vijiji msitengeneze migogoro wala msiwe wabinafsi kwenye maswala ya ardhi, ninyi muwe suluhisho la migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji, si chanzo cha matatizo, wajibu wenu ni kuhakikisha wananchi wanapata haki na migogoro ya ardhi inatatuliwa kwa amani,” alisema Kasilda.
Kijiji cha Marwa kina vitongoji vinne, ambapo kitongoji cha Lesirwai, chenye kaya zaidi ya 200, kipo umbali wa zaidi ya kilomita 25 kutoka makao makuu ya kijiji.
Umbali huo umewafanya wakazi wa kitongoji hicho kushindwa kupata huduma muhimu za kijamii na hata kushiriki mikutano ya kijiji yenye kutoa maamuzi muhimu ya maendeleo hali inayowafanya kuomba kitongoji hicho kupandishwa hadhi na kuwa kijiji.
Kutokana na changamoto hiyo ya umbali wa kufika katika kitongoji hicho, mkuu wa wilaya amewataka wenyeviti wa serikali za mitaa kuhakikisha kuwa wanawafikia wananchi wote, bila kujali umbali wa vitongoji vyao.
Aidha amesisitiza kuwa viongozi wa vijiji wanapaswa kuwajibika kwa kuhakikisha kuwa wanatatua kero za wananchi badala ya kuwa sehemu ya matatizo yanayowakabili.
“Haiwezekani wananchi washindwe kushiriki maamuzi kwa sababu ya umbali, viongozi wa Serikali za mitaa lazima muwafuate wananchi popote walipo ndicho alichotutuma Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwafuata wananchi na kuwapa kwa usawa,” aliongeza Kasilda.
Januari 16 baadhi ya wananchi wa kitongoji cha Lesirwai walifika ofisini kwa Mkuu wa Wilaya na kuomba kubadili matumizi ya ardhi katika eneo wa kitongoji hicho kutoka kuwa la mifugo hadi kuwa la kilimo jambo ambalo Kasilda ameridhia kutokana na wananchi wa kitongoji hicho kutokuwa na idadi kubwa ya mifugo.
Aidha, wananchi wametakiwa kuwa na utulivu wakati serikali inaendelea kushughulikia maombi yao ya kuomba kitongoji hicho kiwe kijiji kamili na kamewataka wananchi wa kijiji cha Marwa kwa ujumla kuacha kukata mapori kutokana na eneo hilo kuwa ni eneo tengefu endapo utafanyika uharibifu katika mapori hali hiyo itaathiri matokeo.
Hatua hii inalenga kuimarisha utawala bora na mshikamano baina ya jamii, hasa katika maeneo yenye changamoto za ardhi. Wananchi wanatarajiwa kushirikiana na viongozi wao kwa karibu ili kuhakikisha kuwa migogoro ya ardhi inatatuliwa kwa njia ya amani na kwa mujibu wa sheria zilizopo.