Simba yatua Azam ikitaka kung’oa kiungo wa kazi

BAADA ya Yanga kutwaa taji la 30 la Ligi Kuu Bara, vita imebaki kwa mshindi wa pili kati ya Simba na Azam, lakini wakati hilo linaendelea wana Msimbazi wameingiza mguu mmoja kuwabomoa matajiri wa jiji la Dar es Salaam, Azam FC.

Azam FC ipo nafasi ya pili baada ya kukusanya pointi 60 kwenye michezo 27 waliyocheza huku Simba ikiwa nafasi ya tatu baada ya kucheza mechi 26 na kufanikiwa kukusanya pointi 57.

Ipo hivi; Kabla ya vita ya kuwania nafasi ya pili haijaisha, baadhi ya watu wa karibu na uongozi wa Simba wamependekekeza jina la kiungo wa kazi pale Azam FC, James Akaminko kwa ajili ya usajili wa msimu ujao ili kuboresha eneo la ukabaji.

Simba ambao msimu uliopita walitupa ndoano kwa kiungo mwingine wa Azam FC, Sospeter Bajana na kukwama katika dakika za mwisho mwisho, lakini msimu huu jicho  lao limeangukia kwa Akamikho ambaye amekuwa bora katika eneo la kiungo mkabaji.

Chanzo cha kuaminikia kutoka ndani ya Simba kimeiambia Mwanaspoti kwamba jina la kiungo huyo Mghana ni miongoni mwa majina yaliyopendekezwa kwenye usajili wa dirisha lijalo na watu wanaoshughulikia ishu za usajili Msimbazi.

“Simba wana mpango wa kusajili mshambuliaji, beki wa pembeni, kiungo na mshambuliaji mmoja wote kutoka nje (ya nchi) na jina la Akaminko limetajwa na linaendelea kufanyiwa kazi. Suala la kumsainisha au kushindwa hilo litajulikana mwisho wa dirisha,” kilisema chanzo hicho.

“Kwenye dirisha la usajili mapendekezo yanakuwa zaidi ya matatu kila eneo, hivyo kupendekezwa kwa wachezaji sio wote wanaweza kusajiliwa, lakini ni lazima mmoja kati yao apewe mkataba.”

AKAMINKO vs AZAM
Kiungo huyo bado ana mkataba na Azam FC hadi 2026 baada ya kumuongezea mwingine kipindi ambacho Yanga walituma ofa ya kumtaka mchezaji huyo.

Chanzo kutoka ndani ya Azam FC kimeiambia Mwanaspoti kuwa mchezaji huyo ameufuata uongozi wa timu hiyo kuomba kuondoka kutokana na kukosa nafasi ya kucheza mara kwa mara, ambapo eneo lake wamekuwa wakitumika Bajana, Yahya Zayd, Yanick Bangala na Adolf Mtasigwa.

“Akaminko amewaomba viongozi kuondoka ili akajaribu maisha mengine nje ya Azam FC na viongozi wamemtuma kwa kocha ambapo (kocha, Youssouph Dabo) amekiri kuwa bado ana mpango naye,” kilisema chanzo hicho.

“Suala la kiungo huyo kuomba kuondoka ni kutokana na namna ambavyo kocha Dabo kashindwa kumpa nafasi ya kucheza akimuamini zaidi Bajana kwenye eneo la kiungo.”

Zayd ambaye amekuwa akitumika eneo hilo kwa sasa kutoka winga, lakini kati ya wachezaji hao chaguo la kwanza ni Bajana ambaye mara nyingi amekuwa akicheza sambamba na Bangala.

Wakati Akaminko anatajwa kutakiwa na Simba kikosi hicho cha Msimbazi katika eneo la kiungo mkabaji kuna Sadio Kanoute, Fabrice Ngoma, Mzamiru Yassin, Abdallah Hamis na Babacar Sarr ambaye anatajwa kuondoka kupisha usajili wa kiungo mpya.

Alipotafutwa kuzungumzia ishu ya Akaminko, Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Popat amesema ni mapema sana kuzungumzia suala la wachezaji kutakiwa na timu nyingine walio kwenye mikataba na kwamba hilo litazungumzwa mwisho wa msimu baada ya timu kufanyiwa tathmini.

“Wachezaji ni wengi wameomba kuondoka, lakini hilo ni suala lililo ndani ya uongozi kwani bado wana mikataba na timu, hivyo mara baada ya msimu kumalizika na kocha kufanya tathmini ya kikosi chake kutakuwa na majibu mazuri nani anaondoka nani anabaki,” amesema Popat.

Alipouulizwa kuhusu taarifa za kiungo huyo kuomba kuondoka, Dabo amesema nachojua ni kwamba Akaminko ni mchezaji wa Azam FC na ndio maana amekuwa akimtumia kwenye kikosi chake.

“Anaondoka anakwenda wapi wakati bado ana mkataba na timu? Nina mpango naye na ndio maana nimekuwa nikimtumia kwenye kikosi changu, suala la kuondoka linaamuliwa na mkataba, lakini mimi taarifa nilizonazo ni mchezaji wa Azam FC kwa mujibu wa mkataba,” amesema kocha huyo.

Hata hivyo, Mwanaspoti ina uhakika kwamba mezani kwa viongozi wa Simba jina la Akaminko lipo na mjadala juu ya usajili wake unaendelea, ingawa bado hawajapeleka ofa katika timu ya Azam FC.

Tangu Bajana alipoumia kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania uliochezwa Desemba 11, 2023 kwenye Uwanja wa Azam Complex timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1, Akaminko ndipo alianza kupata nafasi ya kucheza.

Related Posts