Unguja. Licha ya kutangaza dhamira yake ya kugombea urais Zanzibar, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Zanzibar, Said Mzee Said amesema bado msimamo wa chama hicho upo palepale bila ya kuwepo kwa mabadiliko ya sheria na mifumo hakutakuwa na uchaguzi wa Tanzania.
Said anatangaza nia ya kugombea nafasi ya urais kuvaana na Dk Hussein Mwinyi (CCM) ambaye tayari ameshapitishwa na chama chake kuwania nafasi hiyo kwa awamu ya pili.
Dk Mwinyi ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar kwa sasa, alipitishwa kuwania nafasi hiyo katika Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Januari 18 na 19, 2025 jijini Dodoma ambao pia ulimpitisha Samia Suluhu Hassan kuwania nafasi hiyo kwa upande wa Tanzania bara.
Mbali na Dk Mwinyi, Said pia atachuana na Othman Masoud wa ACT-Wazalendo ambaye naye tayari ameshatangaza nia ya kuwania nafasi hiyo akisema yupo tayari iwapo chama chake kitamteua kuwania nafsi hiyo.
Othman ambaye ni Mwenyekiti wa ACT Wazalendo pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, alitangaza nia yake Januari 1, 2025 alipozungumza na waandishi na wahariri wa vyombo vya habari mjini Unguja.
Akizungumza jana jioni Januari 27, 2028 na wanachama wa chama hicho makao makuu ya Chadema Zanzibar, baada ya kupokewa tangu alipochaguliwa kushika nafasi hiyo katika mkutano mkuu wa chama hicho uliofanyika Januari 21 jijini Dar es Salaam, Said amesema atawania nafasi hiyo licha ya changamoto zinazojitokeza.
“Nimeamua kutangaza nia ya kuwania urais Zanzibar ili kuleta mabadiliko katika Taifa letu,” amesema.
Kwa mujibu wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 ulimuweka madarakani Dk Mwinyi kwa kura 380,402 sawa na asilimia 76.27, mgombea wa Chadema, Issa Mohamed alipata kura 1,702 sawa na asilimia 0.45 huku mgombea wa ACT Wazalendo Maalim Seif Sharif Hamad (marehemu) alipata kura 99,103 sawa na asilimia 19.87.
Said amesema kama kuna nia ya kweli ya kubadilisha mifumo hiyo, wanaweza kusogeza mbele uchaguzi hata miezi sita ili kupisha mifumo mizuri ya kiuchaguzi na haki.
“Bado tunasisitiza msiamamo wa chama, mabadiliko ni muhimu, inaweza kusubiriwa hata miezi sita ili kuwe na uchaguzi mzuri,” amesema.
Amesema kuwachukua wakurugenzi wa halmashauri na kuwaingiza kama watendaji wa uchuguzi, ni moja ya kuharibika kwa uchaguzi huo kwa vile wakurugenzi hao wamechaguliwa na Rais mwenyewe.
“Chadema tunahitaji uchaguzi huru ili kila mshindi aliyeshinda atangazwe kwa mujibu wa sheria sio ubabaishaji,” amesema.
Kuhusu kauli iliyotolewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla hivi karibuni katika ziara yake kisiwani humo, kwamba chama hicho hakina fedha ndio maana kinasingizia mabadiliko, Said amesema chama hicho kina fedha za kutosha isipokuwa kinataka kusimamia demokrasia.
Said ambaye pia alitangaza nia yake ya kuwania urais upande wa Zanzibar licha ya mchakato wa ndani ya chama kuwapata wagombea ukiwa bado, amesema kimejipanga katika kuhakikisha kinashinda uchaguzi ili kushika dola.
“Tupo tayari kujiunga na chama chochote kushirikiana lakini lazima kuwe na nidhamu nzuri kwa masilahi ya wananchi na Taifa letu,” amesema.
Naibu Katibu mkuu wa chama hicho, kwa upande wa Zanzibar, Ali Ibrahim Juma amesema malengo ya chama hicho kwa upande wa Zanzibar ni kukiimarisha ili kushinda uchaguzi na kuchukua dola.
Amesema malengo hayo hayatofikiwa ikiwa wanachama wa chama hicho hawatakuwa kitu kimoja katika kukijenga chama hicho kwa kuwa ni chama imara cha siasa hujengwa na wafuasi wake imara.
“Tunatambua bila ya kuwa na wafuasi imara wa chama itakuwa vigumu kushinda katika uchaguzi, hivyo wakati umefika kwa wanachama wa chama hicho kuwa kitu kimoja ili kushinda dola,” amesema.