Adaiwa kujinyonga kisa kuachwa na mpenzi wake

Arusha. Elirehema Mollel (32) mkazi wa Oldadai mkoani Arusha anadaiwa kujinyonga kwa kile kinachodaiwa kuachwa na mpenzi wake ambaye ni mwanafunzi wa chuo.

Elirehema amekutwa akining’inia juu ya kamba katika nyumba anayoishi.

Akizungumza leo Januari 28, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Justine Masejo amesema mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mount Meru.

“Upelelezi wa tukio hilo unaendelea ili kubaini chanzo halisi cha tukio hilo na kama waliotekeleza waweze kuchukuliwa hatua za kisheria,” amesema.

Baba wa marehemu, Ernest Mollel amesema hivi karibuni binti huyo amekuwa akija katika nyumba ya mwanaye aliyojenga na kupumzika licha ya kuwa mwanafunzi wa chuo.

Amesema alijaribu kuwaachanisha ili mwanafunzi huyo amalize shule kwanza lakini mwanaye alitishia kujiua endapo uhusiano wao ungetenganishwa.

“Nilitaka kuwasiliana na wazazi wa binti ili baadaye isije kuwa lawama, wakijua uhusiano wao na mimi mzazi niko karibu lakini mwanangu alikuwa anasema mwisho wa uhusiano wao itakuwa mwisho wa maisha yake.

“Vijana hao waliwekeana ahadi nyingi akimaliza chuo waoane lakini nadhani tangu jana hawakuwa sawa na binti alinipigia simu kuwa hayuko sawa na mwenzake na yeye anaondoka, nilimwita mwanangu tuongee nini shida akaahidi kufanya hivyo asubuhi,” amesema Ernest.

 Amesema asubuhi ya leo Januari 28,2025 wakati akijiandaa kwenda kwa mwanaye kujua tatizo la usiku wake ndipo alipopigiwa simu kuwa aende eneo la tukio kwa kuwa, amejinyonga.

“Haraka niliwahi eneo la tukio na kukuta kweli mwanangu amejitundika, niliwahi kukata kamba nikidhani naweza kumuokoa lakini kumbe alishafariki,”amesema.

Amesema katika chumba hicho walikuta barua ilivyoandikwa na mwanaye kuwa ameamua kujiua mwenyewe mpenzi wake asilaumiwe kwa chochote, kwa kuwa alikuwa anampenda sana, hivyo uamuzi wa kuachana naye na kuondoka ameona iwe pia mwisho wa maisha yake.

Mkazi wa eneo hilo, Jackson Ally amesema marehemu alikuwa kijana mtiifu na mwenye kutegemewa katika shughuli mbalimbali za vijana.

“Huyu alikuwa hana shida na mtu, ni fundi umeme na amefungua maduka yake mjini huko akifanya biashara na huyu mpenzi wake amekuwa akija hapa mara kwa mara kulala na wamezoeana sana sasa sijui nini kimetokea,” amesema.

Related Posts