Dodoma. Jumla ya Sh97.12 bilioni zinadaiwa na polisi wastaafu, kati ya hizo madai yaliyohakikiwa na kuwasilishwa na Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo ni Sh75.21 bilioni.
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo amesema hayo leo Januari 28, 2025 alipokuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalumu (CCM), Maida Hamad Abdallah aliyehoji ni lini Serikali itawalipa madai ya muda mrefu askari polisi waliomaliza muda wao.
Akijibu swali hilo, Sillo amesema Serikali inaendelea kulipa madai ya askari polisi waliomaliza muda wao wa kazi baada ya kustaafu.
Amesema jumla ya Sh97.12 bilioni zinadaiwa na hadi sasa madai yaliyohakikiwa na kuwasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo ni Sh75.21 bilioni.
“Kwa sasa madai yanayoendelea kuhakikiwa ni ya mwaka wa fedha 2023/24 na kiasi cha Sh21.90 bilioni zinadaiwa. Pindi uhakiki ukikamilika, madai yote yatawasilishwa Wizara ya Fedha kwa ajili ya malipo,” amesema.
Katika swali la nyongeza, Asha Abdallah Juma maarufu Mshua amehoji kuhusu msisitizo wa Serikali katika matumizi ya mfumo wa Teknolojia ya Mawasiliano Tanzania (Tehama) kwa watumishi wote.
“Je, ni kwanini zisiwekwe rekodi vizuri, mfumo huu ukarekodi mahitaji yanayotakiwa kulipwa askari mstaafu, mafao yake na kila kitu chake ile siku ya mwisho anapomaliza kazi badala kumtaka athibitishe alianza lini askari, alipandishwa lini na alikopa kitu gani?” amehoji.
Amehoji kuwa Serikali inafahamu askari hao wanahitaji mafao hayo kuliko siku nyingine.
Akijibu swali hilo, Sillo amesema Jeshi la Polisi liko katika mabadiliko makubwa ya kuweka mfumo wa kieletroniki kwa kuhakikisha taarifa za askari zinaingizwa katika mfumo na kuepuka usumbufu.