Walimu wa sayansi, hisabati wafundwa matumizi ya Tehama

Iringa. Jumla ya walimu wa sekondari 665 wa masomo ya hisabati na sayansi mikoa ya Dodoma, Mbeya na Iringa pamoja na wathibiti ubora (SQA) wapatao 17, wamepatiwa mafunzo ya ufundishaji na ujifunzaji wa masomo kupitia Teknolojia na Habari na Maendeleo (Tehama).

Mafunzo hayo yanayoendeshwa na mradi wa kuimarisha elimu ya sekondari unaotekelezwa na Sequip, Ofisi ya Rais Tamisemi na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, yanalenga kuwanoa walimu katika matumizi ya Tehama kwenye ufundishaji.

Akizungumza leo Jumanne Januari 28, 2025,  Kaimu Ofisa Elimu Mkoa wa Iringa, Reginaldo Msendekwa amewataka walimu hao kuyatumia mafunzo watakayoyapata kuimarisha taaluma ili kuleta maendeleo pamoja na kutumia Tehama katika ufundishaji na ujifunzaji kila siku.

“Dunia inakwenda kwa kasi, masuala ya ufundishaji kwa kutumia mbinu za kizamani yamepitwa na wakati kwa hiyo, tunahitaji walimu wetu wajiimarishe katika ufundishaji kwa kutumia Tehama, zana za kisasa za kisayansi,” amesema Msendekwa.

Msendekwa amesema mafunzo hayo yameandaliwa kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita kwa muda wa miaka mitano kuanzia 2021 hadi 2026.

Mratibu wa mafunzo ya walimu mradi wa Sequip  ya WyEST, Mussa Malalika amesema ni imani yake kuwa walimu hao watafanya vizuri wakirudi katika vituo vyao vya kazi na hilo ndio kusudi la Serikali nchini.

Mkurugenzi msaidizi wa idara ya elimu ya ufundi, Dk Ethel Kasembe amesema mafunzo hayo ni tija katika kuhakikisha sera ya elimu inatekekezwa ipasavyo na kuifanya elimu ya Tanzania kuwa ya vitendo zaidi.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Michael Mvalasau ambaye ni mwalimu wa hisabati Shule ya Sekondari Galigali, ameishukuru  Serikali kwa hatua hiyo ya kuwanoa akieleza yatawasaidia katika shughuli za ufundishaji.

Mafunzo hayo ni ya kwanza kufanyika kwa mikoa hiyo huku katika awamu hii ya pili ya mafunzo yanatarajiwa kufikisha walimu 40,000 wa masomo ya sayansi na hisabati kote nchini.

Related Posts