Sowah, Rupia kuna vita Singida Black Stars

NANI ataongoza safu ya ushambuliaji ya Singida Black Stars? Hicho ndicho kitendawili ambacho kinasubiriwa kuteguliwa na kocha wa timu hiyo, Hamdi Miloud katika mechi za duru la pili kwenye Ligi Kuu Bara.

Miloud anatarajiwa kufanya uamuzi muhimu kuhusu nani atacheza kama mshambuliaji kiongozi kati ya wachezaji wawili hatari alionao kikosini, Elvis Rupia na Jonathan Sowah aliyetua katika dirisha dogo la usajili akitokea Al Nasr ya Libya.

Rupia ambaye ni kinara wa mabao Ligi Kuu Bara akiwa nayo manane atakuwa na kazi ya kulinda nafasi yake dhidi ya ushindani kutoka kwa Sowah ambaye awali alikuwa akiwindwa na Yanga.

Sowah aliyefunga mabao saba katika Ligi Kuu Libya akiwa na Al Nasr msimu wa 2023/24, tayari ameanza kuonyesha uwezo kwenye uwanja na mazoezi wa Singida Black Stars.

Mchezaji huyo ndani ya msimu huo pia alifunga mabao matatu katika Ligi ya Mabingwa Afrika, jambo ambalo linaonyesha ni mshambuliaji wa kiwango cha juu.

Kocha Miloud anatarajiwa kufanya uamuzi mgumu kuhusu nani atakuwa kipaumbele chake cha kwanza kwani kila mmoja kati ya wawili hao ana sifa na uwezo wa kumiliki nafasi hiyo.

Rupia ambaye amezoea mazingira ya ligi amekuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya timu msimu huu.

Hata hivyo, Sowah ambaye amejiunga na Singida Black Stars na matarajio makubwa, amekuwa na mchango muhimu katika mazoezi ya timu na anaonekana kuingia vizuri kwenye mfumo wa kocha.

Akizungumzia ubora wa wachezaji wake kulingana na programu za mazoezi ambazo wamekuwa wakifanya, Miloud alisema: “Nimefurahi kuwa na wachezaji wa kiwango cha juu, kila mmoja wao anajitahidi sana katika mazoezi, na hii inatupa matumaini makubwa kuelea michezo ijayo ya ligi.” Kwa sasa timu hiyo inajiandaa kwa duru la pili la ligi na mashabiki wanatarajiwa kuwaona washambuliaji hao wakiongoza safu ya ushambuliaji kwa pamoja au mmoja kuanza mara kwa mara.

Related Posts