Songwe. Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Songwe limesitisha kazi ya upimaji wa ardhi iliyokuwa likiendelea katika baadhi ya kata wilayani humo.
Hatua hiyo imekuja baada ya wananchi wa kaya 250, kugoma kuondoka katika maeneo wanayoishi kwenye Kitongoji cha Iwindu wakidai ni ardhi yao kihalali.
Akizungumza kwenye kikao cha baraza la madiwani, mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Abraham Sambila amesema Kata ya Ngwala kwa sasa haina amani, hali inayotishia usalama wa baadhi ya viongozi wanaotuhumiwa na wananchi kushiriki katika mpango wa kuwahamisha.
Sambila amesema kutokana na kutokuwepo kwa amani baraza limeazimia kusitisha upimaji huo, kasoro zote zilizojitokeza zirekebishwe, usalama upatikane ndipo kazi iendelee.
Amesema wananchi wapewe elimu ya kujua wanatakiwa wapimiwe maeneo gani na maeneo ya hifadhi ya tambulike.
“Ningefurahi eneo la Muyombo lisitishe maana hili janga litatupeleka pabaya Gua, Ngwala na Kapalala upimaji usitishwe mpaka elimu itakapotolewa kwa wananchi kwani tukiwapa elimu wananchi upimaji utafanyika kwa amani,”amesema Sambila.
Diwani wa Ngwala, Christantus Futakamba ameeleza kuwa anaishi kwa hofu kutokana na tuhuma hizo dhidi ya viongozi akiwamo yeye.
“Watu wanajua mimi ndiye natenga misitu ya hifadhi, wala sio msimamizi mimi ni mshauri wanaotenga ni wananchi na kupitishwa kwenye mkutano wa hadhara, hivyo inapotokea hifadhi zimesitishwa lazima nihoji ili nijue kama kuna mtu anataka kuvamia hifadhi,”amesema Futakamba.
Hivi karibuni wananchi wa Kijiji cha Iwindu katika mkutano wa hadharaa uliofanyika kijijini hapo, walisema wamekuwa wakisumbuliwa mara kwa mara na baadhi ya viongozi kutaka kuwandoa katika eneo hilo bila kuwapa eneo mbadala la kwenda kuishi.
Mayamu Tujimwele, mkazi wa kijiji hicho amesema wanashangazwa kuona wanatolewa katika maeneo ambayo wamelipia wanayoishi kihalali kwa miaka 15.
Emanuel Nzoka, amehoji kuwa kama eneo hilo ni hifadhi kwa nini viongozi wa Serikali ya kijiji wanakwenda kuchukua michango ya maendeleo kwa wananchi bila kuwaandaa na kuwaambia kuwa eneo hilo ni la hifadhi ya kijiji.
Ofisa Ardhi wa Wilaya ya Songwe, Jailo Shukrani amekiri kuwepo kwa taharuki iliyojitokeza kwa wananchi kuhusu uhalali wa kuishi katika maeneo hayo.