Mufindi. Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa amesisitiza viongozi wa halmashauri kuhakikisha mazingira yanayoizunguka Hospitali ya Mji Mafinga yanaendelea kuboresha kwa kupandwa ukoka, miti na maua sanjari na kuweka maeneo kwa ajili ya kupumzika wagonjwa.
Kauli hiyo imetolewa na Dk Salekwa leo Jumanne Januari 18 2025 alipozindua upandaji wa miti katika Halmashauri ya Mji Mafinga uliofanyika katika Hospitali ya Mji Mafinga kwa kushirikisha Kampuni ya Preshdas iliyotoa ya miche 570.
Amesema huduma bora zikitolewa kwa usawa kwa wananchi bila kuwa na matabaka, itawafanya kupata huduma bora na kuisemea Serikali vizuri.
Dk Salekwa amesema Preshdas imekuwa msingi mzuri katika maendeleo ya sekta ya kilimo cha miti na ufugaji nyuki kwa wananchi wa Wilaya ya Mufindi kwa utoaji wa elimu na miongozo mbalimbali inayohusu ufugaji pamoja na mazao hayo.
“Ni muda sasa wa vikundi mbalimbali vilivyopokea mikopo ya asilimia 10 katika Wilaya ya Mufindi kutumia fursa ya uwepo wa kampuni hii kwa ajili ya kupata mafunzo yanayohusu uwekezaji katika sekta kilimo cha miti na ufugaji nyuki,”amesema Dk Salekwa
Ofisa Mafunzo na Rasilimali kutoka Preshdas, Geofrey Nyakunga amesema kampuni hiyo ni mdau wa mazingira hususani katika kilimo cha misitu na sekta ya nyuki, hivyo wananchi wanakaribishwa kwa ajili ya kupata huduma zinazotolewa na kampuni hiyo.
Pia, ofisa huyo amewashukuru Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) kwa kuwaunga mkono katika kampeni hiyo akisema katika miti 500 iliyopandwa katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji Mafinga, 400 imetolewa na wakala huo.
Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Uenezi kutoka Preshdas Elizabeth Mbunda amesema kampuni inatambua umuhimu wa utunzaji wa mazingira, hivyo watashirikiana na wadau wengine kutoa elimu kwa wananchi.
” Tutashirikiana na wadau wengine kutoa elimu kwa wananchi namna ya upandaji wa miti na utunzaji, pamoja na ufugaji nyuki ili iweze kuletwa tija kwa wananchi,” amesema Mbunda.