Dar es Salaam. Familia ya Jumanne Ramadhani aliyefariki kwa madai ya kumwagiwa petroli kisha kuchomwa moto kwa tuhuma za wizi simu na fedha, imeiomba Serikali kuwachukulia hatua za kisheria waliohusika na kitendo hicho ikidai ndugu yao hakuwa mwizi.
Ramadhan aliyekuwa akiishi Mtaa wa Discover, Kimara Suka Manispaa ya Ubungo jijini Dar es Salaam anadaiwa kuchomwa moto Januari 23, 2025 usiku baada vijana watatu kumfuata nyumbani kwake kwa bajaji akawafanyie usafi kwenye nyumba mpya, kisha kumgeuka na kumchoma moto wakimuita mwizi.
Juhudi za kumtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu, Jumanne Muliro kuzungumzia tukio hilo zinaendelea, kwa kuwa simu yake ya mkononi inaita bila kupokewa.
Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Lazaro Twange amesema anafutilia kujua sakata hilo kwa undani, akieleza kwa kuwa kuna madai ya kijinai polisi wanaweza kuzungumzia zaidi.
“Kwangu naomba mnipatie muda nifuatilie…nitakujibu nataka nipate taarifa halisi za nini kilitokea, wamefikia wapi?,” amesema Twange
Akimzungumzia marehemu, Mjumbe wa Mtaa wa Discover, Qwine Kaduma amesema anamfahamu Ramadhani na alikuwa na mke na watoto wawili huku kazi yake ikiwa ni kufanya usafi kwenye nyumba kubwa kubwa.
“Kijana huyo alikuwa mwema, muaminifu, mstaarabu na tangu ameanza kuishi eneo hili sikuwahi kupata taarifa za ovyo kuhusu yeye na nilivyopata taarifa hizo imenishangaza,” amesema.
Qwine amesema alikuwa kijana mwerevu na anayeshirikiana na watu wengi, ndiyo maana wakazi wengi wamejitokeza kwenye msiba wake wakijiuliza maswali mengi.
“Ni muhimu vyombo vinavyohusika vikatenda haki katika kuchunguza jambo hili, wananchi wanajiuliza mengi tangu akiwa mdogo alianza kuishi hapa hajawahi kusikika akifanya mambo ya wizi,” amesema Qwine.
Mke wa marehemu aelezea tukio
Mke wa marehemu, Hellen Dominick amesema mumewe aliyekuwa akiishi naye kwa upendo amemwachia watoto wawili.
“Siku ya tukio, saa tatu usiku mume wangu alikuwa amepumzika kitandani, mimi nilikuwa naangalia runinga mlango ulikuwa umeegeshwa ghafla nikasikia mtu anagonga,” amesema.
Amesema, baada ya kusikia hodi alikwenda kufungua mlango na kuwaona watu wawili na watatu yupo kwenye bajaji walisalimiana kisha walimuulizia mumewe na aliwajibu amepumzika ndani.
“Nilirudi ndani kumwambia mume wangu unaitwa, kweli alitoka hadi nje hapo barabarani walikuwa wanazungumza wenyewe sikuwa najua kinachoendelea na mimi nilitoka kuchungulia baada ya kumaliza alirudi ndani kuchukua simu,” amesema.
Amesema alipomuuliza kuna jambo gani usiku huo kwani si kawaida, mumewe alimjibu ni mabosi zake anaowafanyia usafi walikuja kumchukua kwenda kufanya shughuli hiyo kisha waliondoka.
“Baada ya muda kupita, nilimpigia simu alipokea na kunieleza hatochukua muda atakuwa amerudi lakini nikaona anachelewa nikapiga simu zaidi ya mara 10 hazikupokewa nikaanza kuwa na shaka,” ameeleza.
Baada ya muda, amesema alikuja rafiki yake ambaye ni dereva bodaboda kumpatia taarifa kuwa, muwewe amemuona yupo mtupu na amechomwa moto.
“Ikabidi nitoke nje, kufika nilikutana na wale vijana waliokuja kumchukua akiwamo aliyekuja kugonga mlango wakaniuliza mume wako yuko wapi nikashaanga inakuwaje mnaniuliza wakati mliondoka naye,” amesema.
Amesema baada ya majibizano kwa ujasiri mkubwa walimuambia wamemchoma moto ndipo walipoanza kuvutana na kupigana, alipomuangali mkononi mmoja wao alikuwa ameshika kiberiti mkononi.
“Tulianza kuvutana na kupigana wote wakinishambulia na wakaanza kujaa watu nilipomuuliza kujua kisa cha kumchoma moto nilijibiwa ameiba hela ila kiwango hakijulikani,” amesema.
Amesema baada ya kuwahoji zaidi walidai wameibiwa simu kubwa moja na pochi iliyokuwa na fedha ingawa kiwango chake hakikujulikana.
Amesema wakati majibizano yakiendelea na watu kuzidi kujaa ndipo alikuja bodaboda aliyempeleka Hospitali ya Kimara Mwisho na kushuhudia jinsi mume wake alivyobabuliwa na moto.
“Mume wangu alikuwa amebabuliwa mwili mzima na moto kusema kweli niliumia na nikifikiria yeye ni baba watoto wangu na sina kazi na mtoto wa kwanza ana miaka sita na mwingine mitatu niliumia,” amesema.
Amesema kutokana na majeraha ya moto, alipata rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Mwananyama lakini walipofika ikashindikana ndipo wakaenda Hospitali ya Taifa Muhimbili umauti ulipomkuta.
“Tulienda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikofariki akipatiwa matibabu lakini nikiwa naye kwenye gari ya wagonjwa aliniambia hajachukua chochote na kunitaka niangalie watoto,” amesema Hellen.
“Sijui watoto hawa kuanzia sasa nitawaleaje, sina kazi yoyote mume wangu alikuwa anafanya yote hapa nawaza gharama zilizotumika katika matibabu kwakuwa bili imekuja,” amesema.
Dada wa marehemu, Rehema Ramadhani amesema kaka yake alifariki dunia Januari 24, 2025 akiwa anapatiwa matibabu Hospitali ya Taifa Muhimbili.
“Taarifa za kuchomwa moto kaka yangu nilizipata usiku wa Januari 23, 2025 kutoka kwa wifi yangu aliyekuja nyumbani kunieleza mume wake amepata shida na tukaenda hadi kwa vijana hao kuwauliza, walikiri wamemchoma moto kwakuwa amewaibia tulipowadai ushahidi walibaki kimya,” amesema.
Rehema amesema wanajua alichofanyiwa kaka yake ni uhuni na kuitaka Serikali kufuatilia suala hilo kwa kina ili haki itendeka.
“Tunasubiri taarifa ya Polisi na mambo yakikamilika kwakuwa mwili upo Muhimbili, tunapanga usafirishwe kwenda mkoani Kilimanjaro katika Wilaya ya Same kwenda kuzikwa maeneo ya Hidaru,” amesema.