Dar es Salaam. Baadhi ya madereva wa magari ya mizigo kutoka Tanzania, wamekwama katika mji wa Goma, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), huku Chama cha Wafanyakazi wa Malori Tanzania (Chawamata), kikithibitisha kuwa suala hilo linashughulikiwa kwa umakini mkubwa na Ubalozi wa Tanzania nchini humo.
Jumapili, Julai 26, 2024, waasi wa kundi la M23 walitangaza kulidhibiti jiji la Goma, Mashariki mwa DRC, hali iliyosababisha mapigano makali na kulazimisha zaidi ya watu milioni mbili kukimbia makazi yao.
Serikali ya DRC imelaani kitendo hicho, ikitafsiri hatua hiyo kama tangazo la vita, huku Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) likitoa wito wa kuondolewa kwa waasi na vikosi vya kigeni katika eneo hilo.
Aidha, kiongozi wa Muungano wa Waasi wa Congo River Alliance, Corneille Nangaa ambaye ni mshirika wa karibu wa Sultani Makenga (kiongozi wa wapiganaji wa M23), amesema lengo lao halikuwa tu kuiteka Goma, bali pia mji mkuu wa Kinshasa ili kumuondoa madarakani Rais, Félix Tshisekedi.
Leo, Jumanne, Januari 28, 2025, Mwenyekiti wa Chawamata, Nuhu Mgodoka akizungumza na Mwananchi, amethibitisha kuwa chama hicho kimekuwa na mawasiliano ya karibu na ubalozi wa Tanzania nchini DRC kuhusiana na hilo, akieleza kuwa tayari hatua zimeanza kuchukuliwa ili kuhakikisha madereva waliokwama wanatoka wakiwa salama.
“Tangu tulipopata taarifa hizi tunashirikiana kwa karibu na ubalozi wetu nchini DRC. Wametuhakikishia kuwa kila Mtanzania aliyeko huko atasaidiwa, wakiwamo madereva wenzetu ambao leo Jumanne Januari 28, 2025 video zao zimeendelea kuonekana mitandaoni wakiomba msaada,” amesema Mgodoka.
Kwa mujibu wa Mgodoka, mpaka sasa idadi ya madereva waliokwama Goma ilikuwa 43. Hata hivyo, amesema wanaweza kuwa zaidi ya 50, kwa sababu baadhi ya madereva walikuwa maeneo mengine, ikiwemo Jambo Safari.
Katika video iliyosambaa mitandaoni, mwanaume mmoja anasikika akiomba msaada akiwa chini ya uvungu wa gari, akieleza kuwa wako karibu na uwanja wa ndege wa Goma, jirani na kambi za jeshi la UN na Monusco.
“Hatuna mtu wa kutusaidia. Tunaomba jamani, mrushe kwenye magrupu hata jeshi letu litusaidie. Tupo jirani sana na Monusco, lakini hatuna mawasiliano nao. Tunaomba msaada, tupo Watanzania 43, na hatujui nani anakuja kututoa huku,” alisikika akisema mwanaume huyo huku milipuko inayosadikiwa ni ya mabomu ikisikika pia.
Mmoja wa madereva aliyezungumza na Mwananchi kwa simu kutokea Goma, William Mwajeka amesema hali ni mbaya eneo alipo akibainisha kuwa amekuwa ndani ya gari kwa siku tatu bila kushuka.
“Hapa nilipo, mingurumo ya risasi inasikika kila mara kwa sababu mapigano yanaendelea. Hali ni mbaya sana,” amesema Mwajeka.
Amesema yupo karibu na kambi ya jeshi na mashambulizi yanaendelea, huku mabomu yakipigwa na vipande vya mabati na chuma vinavyopasuka vikidondoka juu ya gari lake, jambo ambalo linamfanya kuwa na hofu kuhusu usalama wake.
“Nilipewa namba za kupiga ubalozini ili nipate msaada, lakini niliyempata kwenye simu alinijibu nitafute bodaboda ili nikimbilie walipo wenzangu. Kwa hali ilivyo, haiwezekani kabisa kutumia usafiri wa bodaboda au kufika kokote,” amesema.
Abdallah Msalu, dereva kutoka kampuni ya Kii Star, amesema vurugu hizo zilianza siku nne zilizopita, lakini hali ilizidi kuwa mbaya zaidi jana kuanzia asubuhi hadi usiku wa kuamkia leo. Msalu, aliyekuwa na mwenzake aliyemtaja kwa jina moja la Stephano, amesema walikutana na waasi njiani wakiwa wanarudi.
“Waasi walituzuia na kutaka tuwape hela. Tulitoa fedha tulizokuwa nazo, nao wakaturuhusu kuondoka. Tulipofika kwenye geti la mpaka kati ya Congo na Rwanda, vurugu kati ya waasi na askari wa Jeshi la UN zilianza,” amesema Msalu.
Kwa sasa, Msalu na wenzake wapo Rwanda wakisubiri maelekezo zaidi, kwani hati zao za kusafiria hazijapigwa muhuri baada ya maofisa wa mpaka kukimbia mapigano.
Wamiliki wa malori watoa neno
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori ya Kati na Wadogo (Tamstoa), Chuki Shabani amesema wanawasiliana na madereva walioko nchini DRC.
“Leo saa tisa mchana, wamethibitisha kuwa mapigano yalikuwa yamepungua kidogo, lakini wananchi waliokuwa eneo hilo walikuwa wakiwapora madereva mali zao,” amesema Chuki.
Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa, amethibitisha kuwa Serikali imepata taarifa za tukio hilo na inafuatilia kupitia ubalozi wa Tanzania uliopo DRC, ili kuangalia njia bora ya kuwasaidia Watanzania waliokwama.
“Changamoto kubwa ni kwamba eneo hilo liko katikati ya mapigano, hivyo si rahisi kuingia na kuwatoa watu. Hata hivyo, tunatafuta njia bora ya kuhakikisha Watanzania wote wanatolewa salama,” amesema Msigwa.