Dodoma. Bodi ya Bima ya Amana (DIB), imewalipa wateja 1,391 kati ya 2,797 wa Benki ya Wakulima Kagera (KCB), waliokuwa na amana chini ya Sh1.5 milioni.
Naibu Waziri wa Fedha, Hamad Chande amesema hayo leo Jumanne Januari 28, 2025 wakati akijibu swali la Bernadeta Mshashu aliyehoji lini Serikali itawalipa wateja walioweka fedha zao katika benki hiyo.
Akijibu swali hilo, Chande amesema Januari 4, 2018, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), iliifutia leseni ya biashara benki hiyo na kuiteua Bodi ya Bima ya Amana kuwa mfilisi wa benki hiyo.
Amesema hadi Desemba 2024, jumla ya Sh846.16 milioni kati ya Sh899.56 milioni sawa na asilimia 94.06 zimelipwa kama fidia ya bima ya amana kwa wateja 1,391 waliojitokeza kati ya wateja 2,797 waliokuwa na amana isiyozidi Sh1.5 milioni.
Aidha, katika kipindi hicho, bodi ya Amana imelipa wadai wa benki fidia ya ufilisi Sh664.25 milioni kati ya madai ya Sh1.64 bilioni sawa na asilimia 40.50 ya wateja 195 kati ya wateja 274 wanaostahiki kulipwa fidia hiyo.
“Ninatoa rai kwa mheshimiwa mbunge kuhamasisha wananchi wanaodai fedha zao kuwasiliana na Bodi ya Bima ya Amana,” amesema.
Katika swali la nyongeza, Mshashu amesema kwa kuwa ni miaka minane sasa tangu benki ya Wakulima Kagera kufungwa, wateja waliokuwa na amana ya zaidi ya Sh1.5 milioni wamelipwa asilimia 43 ya fedha zao walizokuwa wameweka benki.
“Ni lini Serikali itawalipa watu hao asilimia 57 ya fedha zao zilizobaki benki kwa sababu wanateseka? Kwa kuwa watumishi wa benki hiyo walilipwa nauli tu, hawakulipwa stahiki zao ni lini stahiki zao zitalipwa?” amehoji.
Akijibu swali hilo, Chande amesema malipo ya watu hao yanaendelea kulipwa, hivyo waendelee kuhamasisha wawasiliane na Bodi ya Bima ya Amana ili kulipwa madai yao.
“Lakini kuhusu suala la watumishi haya ni masuala ya kiutumishi, naomba tulichukue nikae naye na watu wa utumishi ili tuweze kuwasaidia watu wetu hao,” amesema.